Saturday, June 30, 2018

IFAHAMU SHERIA YA MTOTO YA MWAKA 2OO9 (THE LAW OF THE CHILD ACT, 2009) [SEHEMU YA SITA]



SURA YA NANE

KULEA MTOTO

Nani anaweza kuwa mlezi?
(i) Mtu yeyote mwenye umri juu ya miaka ishirini na moja, mwenye maadili mema na tabia njema, anaweza kuwa mlezi wa mtoto.
(ii) Mlezi, kama ilivyotumika katika sehemu hii, ni mtu ambae siyo mzazi wa mtoto lakini ana hiari na uwezo wa kumtunza na kumkimu mtoto.
(iii) Kamishna anaweza kumweka mtoto chini ya mlezi pale:
(a) Mtoto anapopelekwa katika makazi yaliyoidhinishwa au taasisi chini ya amri ya
usimamizi;
(b) Mapendekezo yanapofanywa na Ofisa wa Ustawi wa Jamii kwamba makazi
yaliyoidhinishwa au taasisi ni mahali panapomfaa mtoto; au
(c) Mtoto anapokuwa amewekwa na mtu yeyote katika makazi yaliyoidhinishwa au taasisi.
(iv) Maombi ya kumlea mtoto yatafanywa kwa Kamishna, ambaye atayapeleka kwa Ofisa waUstawi wa Jamii, mlezi au mtu aliye na mamlaka katika makazi yaliyoidhinishwa.
(v) Mlezi ambaye mtoto amewekwa chini ya matunzo na malezi yake atakuwa na majukumu ya kumlea na kumkimu mtoto sawa na majukumu aliyonayo mzazi wa mtoto.
(vi) Mtoto aliyewekwa chini ya malezi atakuwa na haki ya kuabudu kulingana na imani ya dini yake wakati alipozaliwa.
(vii) Mlezi anayekiuka sheria kama ilivyoainishwa sehemu hii atakuwa ametenda kosa chini ya sheria hii.


SURA YA TISA52
KUASILI MTOTO
Kutoa Amri ya Kuasili
Maombi ya kuasili yanafanywa wapi?
(i) Kwa kuzingatia sheria kama ilivyoainishwa katika
Sheria hii:
(a) Maombi ya kuasili mtoto yanaweza kufanywa Mahakama Kuu;
(b) Maombi kwa ajili ya “kuasili kwa wazi” yatafanywa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi au Mahakama ya Wilaya.
(ii) Baada ya kupokea maombi, Mahakama inaweza kutoa amri ya kuruhusu maombi ya kuasili au kuasili kwa wazi kulingana na Sheria hii.
(iii) Maana ya kuasili kwa wazi” kama ilivyotumika katika sheria hii, ni kuasili mtoto kunakofanywa na ndugu.
53
Ni nani anaweza kuomba kuasili?
Maombi ya kuasili
(i) Maombi ya amri ya kuasili yanaweza kufanywa kwa pamoja na
(a) Mume na mke; au
(b) Mama au baba wa mtoto peke yake au pamoja na mwenzi wake.
(ii) Kuhusu maombi ya kuasili kwa wazi, maombi hayo yanaweza kufanywa na ndugu wa mtoto.
54
Ridhaa ya Wazazi na Walezi
(i) Amri ya kuasili itatolewa tu kunapokuwa na ridhaa ya wazazi au walezi wa mtoto.
(ii) Mahakama inaweza kutohitaji ridhaa ya wazazi, walezi au ndugu wa mtoto kama itaridhika kwamba:
(a) Wazazi, walezi au ndugu wamemtelekeza mtoto au wamekuwa wakimtendea mtoto vibaya kwa muda mrefu.
(b) Au kama mtu hawezi kupatikana au hana uwezo wa kutoa ridhaa.
(c) Au kama hakuna sababu ya maana ya kutokutoa ridhaa.
(iii) Mzazi yeyote, mlezi au ndugu wa mtoto ambaye anahusika katika maombi ya kuasili au ametoa ridhaa kwa ajili ya amri ya kuasili hatastahili kumtoa mtoto kutoka kwa mwombaji. Itakuwa hivyo tu kama ana kibali cha mahakama na itakuwa kwa manufaa ya mtoto.

Amri ya kuasili
Je, mtoto aliyeasiliwa ana haki ya kupewa taarifa ya uasili?
(i) Mzazi aliyeasili atamfahamisha mtoto aliyeasiliwa kwamba ameasiliwa. Atamfahamisha pia kuhusu nasaba yake. Lakini, taarifa hii itatolewa kama:
(a) Ni kwa ajili ya manufaa ya mtoto; na
(b) Mtoto ana umri angalau wa miaka kumi na nane.
(ii) Mtu mwingine hana ruhusa ya kutoa taarifa kwamba mtoto ameasiliwa isipokuwa mzazi wa kuasili.
(iii) Mtu yeyote anayekiuka kifungu hiki anatenda kosa. Akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini ya si chini ya shilingi mia moja elfu, lakini isiyozidi shilingi milioni mbili au kifungo cha muda usiozidi miezi kumi na mbili au vyote kwa pamoja.
Maombi yaliyofanywa na Mtu Asiyekuwa Mkazi
(i) Katika maombi ya kuasili yaliyofanywa na mwombaji ambaye ni raia wa Tanzania, lakini haishi ndani ya Tanzania, mahakama itajiridhisha kwamba kuna taarifa za kutosha kuweza kufanya maombi, kisha itatoa amri ya muda.
Vilevile, kama maombi ya pamoja yamefanywa, na mmoja wa waombaji si mkazi wa Tanzania, mahakama itajiridhisha kwamba kuna taarifa za kutosha kuweza kufanya maombi, kisha itatoa amri ya muda.
(ii) Mahakama itajiridhisha kwamba kuna taarifa za kutosha kutoka kwa mamlaka inayotambulika kule mwombaji anakoishi na kwenye nchi yake ya asili, ndipo itoe amri ya muda au amri ya kuasili.
 
Watoto ambao waliasiliwa kabla
(i) Amri ya kuasili au amri ya muda inaweza kufanywa kwa ajili ya mtoto ambaye ameshaasiliwa na wazazi wa kuasili . Kama wazazi wa kuasili wa awali bado wako hai, watachukuliwa kuwa ni wazazi au walezi wa mtoto kwa lengo la kuasili kunakofuata.

Athari za Kuasili kwa haki za Mzazi
 (i) Wakati amri ya kutoa amri ya kuasili:
(a) Haki, wajibu na majukumu yanayotokana na kuasili yana ukomo. Haya ni pamoja na yale yanayotokana na sheria za mila na desturi za wazazi wa mtoto, au mtu yeyote anayehusiana na mtoto.
(b) Haki, wajibu na majukumu ya wazazi vitakuwa chini ya mzazi wa kuasili ambaye anachukua nafasi ya mzazi wa mtoto. Hii inajumuisha majukumu yote kuhusu uangalizi, kukimu na elimu ya mtoto, kama vile mtoto alizaliwa na wazazi wa kuasili kisheria katika ndoa yao, na hakuwa mtoto wa mtu mwingine .
(ii) Pale ambapo amri ya kuasili imetolewa kwa mume na mke kwa pamoja, wote kwa pamoja watachukua majukumu ya wazazi kama vile wamemzaa mtoto wao wenyewe kiasili kama mume na mke.
 
Kuasili na Sheria za Kimila
(i) Mtoto wa kuasili atakuwa chini ya sheria za kimila kama vile alikuwa mtoto wa kuzaliwa wa wazazi wa kuasili kama wazazi wa kuasili wako chini ya sheria za kimila.

Usajili wa Watoto Walioasiliwa
(i) Amri ya kuasili iliyotolewa na mahakama itakuwa na maelekezo kwa Msajili Mkuu kuweka kumbukumbu katika Rejesta ya Watoto Walioasiliwa.
(ii) Kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya kumbukumbu ya rejesta, ambapo:
(a) Tarehe halisi ya kuzaliwa mtoto haijathibitika kuweza kuiridhisha mahakama, mahakama itaamua tarehe inayoelekea kuwa tarehe ya kuzaliwa kwa mtoto. Tarehe hiyo itatajwa kwenye amri.
(b) Jina au ubini litakalotumika kwa mtoto likiwa tofauti na lile la awali, jina jipya litatajwa kwenye amri badala ya jina la zamani.
(c) Nchi aliyozaliwa mtoto haijathibitika kuweza kuiridhisha mahakama, taarifa za nchi hiyo zinaweza kuachwa katika amri ya kuasili. Nchi haitawekwa pia kwenye Rejesta ya Watoto Walioasiliwa.
(iii) Kwa mtoto ambaye alikuwa hajaasiliwa, maelezo ya kwamba “Ameasiliwa” yatatolewa kwa Msajili Mkuu na kuwekwa kwenye taarifa za Rejesta ya Vizazi. Hili litafanyika baada ya mahakama kupokea maombi ya amri ya kuasili na kujiridhisha kwamba taarifa zinaendana na zile zilizo kwenye Rejesta ya Vizazi.
(iv) Pale ambapo amri ya kuasili imetolewa na mahakama chini ya sheria hii, mahakama itawasilisha maelekezo kwa Msajili Mkuu. Baada ya kupokea mawasiliano hayo,Msajili Mkuu atawezesha maelekezo yaliyoko kwenye amri ya mahakama yatekelezwe yote. Neno “Ameasiliwa” litawekwa kwenye Rejesta ya Vizazi na katika Rejesta ya Watoto Walioasiliwa.

Kuasiliwa na Mtu Asiye Raia
Je, mtoto anaweza kuasiliwa na mtu ambaye sio Mtanzania?
(i) Mtu yeyote ambaye siyo raia wa Tanzania anaweza kuasili mtoto ambaye ni Mtanzania. Hilo linawezekana kama:
(a) Mtoto hawezi kuwekwa chini ya malezi au kwenye familia ya kuasili. Au kama mtoto hawezi kutunzwa katika hali ambayo inafaa kwa ajili ya ustawi wake akiwa Tanzania.
(b) Mtu anayetaka kuasili ameishi Tanzania kwa muda wa miaka mitatu mfululizo;
(c) Amemlea mtoto kwa muda wa miezi mitatu chini ya usimamizi wa Ofisa Ustawi wa Jamii;
(d) Hana historia ya kutenda makosa ya kijinai katika nchi aliyotoka au nchi nyingine yoyote;
(e) Amependekezwa kuwa anafaa kumuasili mtoto kutoka kwa Ofisa wa Ustawi wa Jamii. Au kama amependekezwa na mamlaka yenye uwezo katika nchi ambako anaishi.
(f) Ameiridhisha mahakama kwamba nchi alikotoka inaheshimu na inatambua amri ya
kuasili.
(ii) Kwa kuzingatia kifungu kidogo cha (i) , mahakama inaweza kutoa amri ya kuasili
kama ni kwa ajili ya manufaa ya mtoto.
(iii) Kwa ajili ya maombi ya kuasili ya mtu ambaye sio raia wa Tanzania, Ofisa Ustawi wa Jamii atatakiwa kufanya uchunguzi. Ofisa wa Ustawi wa Jamii atatoa ripoti ya uchunguzi wa kijamii ili kuisaidia mahakama kufanya uamuzi kuhusu maombi.
(iv) Mahakama inaweza kutoa amri ya ziada kuhusiana na maombi ya kuasili ya mtu
asiye raia wa Tanzania:
(a) Kumtaka Ofisa wa Ustawi wa Jamii kuwakilisha maslahi ya ustawi wa mtoto;
(b) Kumtaka Ofisa wa Ustawi wa Jamii kuandaa ripoti ya uchunguzi wa kijamii ili kuisaidia mahakama kufanya maamuzi, iwapo amri ya kuasili itakuwa kwa manufaa ya mtoto au la;
(c) Suala lolote ambalo mahakama inaweza kuamua.

Friday, June 29, 2018

IFAHAMU SHERIA YA MTOTO YA MWAKA 2OO9 (THE LAW OF THE CHILD ACT, 2009) [SEHEMU YA TANO]



SURA YA TANO
UZAO
Maombi ya Nasaba
Kama baba wa mtoto hajulikani, nani anaweza kuomba uthibitisho wa uzao?
(i) Wafuatao wanaweza kuomba mahakamani amri ya kuthibitisha uzao wa mtoto:
(a) Mtoto;
(b) Mzazi wa mtoto;
(c) Mlezi wa mtoto;
(d) Ofisa wa Ustawi wa Jamii; au
(e) Kwa ruhusa rasmi ya mahakama, mtu yeyote mwenye kuvutiwa na mtoto.

(ii) Ni wakati gani maombi yanaweza kufanywa
mahakamani ?
(a) Kabla mtoto hajazaliwa;
(b) Baada ya kifo cha baba au mama wa mtoto;
(c) Kabla mtoto hajafikisha umri wa miaka kumi na nane. Inawezekana pia, kwa ruhusa rasmi ya mahakama, kuomba amri ya kuthibitisha uzao baada ya mtoto kufikisha umri wa miaka kumi na nane.

Ushahidi wa Nasaba
(i). Ushahidi wa uzao wa mtoto unatokana na nini?
(a) Ndoa yoyote iliyofungwa kwa kufuata Sheria ya Ndoa;
(b) Jina la mzazi kuingizwa katika rejesta ya vizazi inayotunzwa na Msajili Mkuu;
(c) Kufanywa kwa sherehe ya kimila na baba wa mtoto;
(d) Kutambuliwa na jamii kwa uzao huo: na
(e) Matokeo ya vipimo vya vinasaba.

Vipimo vya Nasaba ni nini?
Hivi ni vipimo ambavyo vinatoa ushahidi thabiti juu ya uzao wa mtoto. Baba anayedhaniwa kuwa baba mzazi anapimwa vipimo vya nasaba ili kuwa na uhakika kwamba yeye ndiye baba mzazi. Nasaba hupatikana katika kiini cha seli hai na huwa na taarifa za urithi kutoka kwa mzazi kwenda kwa mtoto. Taarifa za nasaba ndizo pekee zenye kutoa ukweli usiopingika kuhusu uzao wa mtoto.
40
Vipimo vya Kidaktari
(i) Mahakama inaweza kutoa amri, kwa anayesemekana kuwa ni baba mzazi wa mtoto, kupeleka vipimo vya kidaktari. Kwa kutegemea na ushahidi utakaopatikana kutokana na vipimo, mahakama itatoa amri kama inavyoona inafaa.
(ii) Pamoja na vipimo vya kidaktari, pale ambapo ushahidi wa mama au ushahidi mwingine wowote unaojitegemea haulingani/haufanani na ushahidi uliopatikana kutokana na vipimo, mahakama yenyewe, inaweza kuamuru vipimo vya vinasaba vifanywe kwa nia ya kuthibitisha baba mzazi wa mtoto.
Au, maombi ya vipimo vya kinasaba yanaweza kupelekwa mahakamani.
(iii) Mahakama itaamua na kutoa amri nani atalipia gharama kuhusiana na vipimo vya vinasaba.
(iv) Pale mahakama inapotoa amri kuhusu baba mzazi, baba huyu atachukua majukumu kwa mtoto kama vile anavyowajibika kwa mtoto aliyezaliwa ndani ya ndoa. Mtoto naye, kwa kuzingatia dini ya baba mzazi, atakuwa na haki zote kutoka kwa baba pamoja na haki ya urithi.
42
SURA YA SITA

UANGALIZI NA NJIA YA KUMTEMBELEA MTOTO

Nani anaweza kuwa mwangalizi wa mtoto?
(i) Mzazi, mlezi au ndugu anayemtunza mtoto anaweza kuomba mahakamani kuwa mwangalizi wa mtoto.
(ii) Mahakama inaweza kutoa amri ya kuishi na mtoto kwa mwombaji kuwa mwangalizi, kwa masharti itakayoona yanafaa. Hili litategemea mwenendo wa maombi ya kuthibitisha uzao wa mtoto.
(iii) Mahakama inaweza, wakati wowote, kufuta amri ya kuishi na mtoto kama mwangalizi kwa mtu na kumpatia mtu mwingine majukumu hayo.
Majukumu hayo yanaweza pia yakapatiwa makazi yaliyoidhinishwa au taasisi, kama mahakama ikiona ni lazima.
(iv) Katika kufikia maamuzi ya kutoa amri ya kuwa mwangalizi wa mtoto au kufuta amri hiyo, mahakama itazingatia kwanza furaha na amani ya mtoto.
43
Kumtembelea mtoto
Mzazi, mlezi au ndugu ambaye amefutiwa amri ya kuwa mwangalizi wa mtoto anaweza kuomba mahakamani kupata nafasi ya kumtembelea mtoto kwa vipindi maalumu.

Uamuzi juu ya Kumtembelea Mtoto
(i) Mahakama itazingatia furaha na amani ya mtoto na umuhimu wa mtoto kuwa na mama yake wakati inapotoa amri ya uangalizi wa mtoto na kumtembelea mtoto.

(ii) Wakati wa kutoa amri ya uangalizi, mahakama inazingatia nini?
(a) Haki za mtoto;
(b) Umri na jinsia ya mtoto;
(c) Kama inafaa mtoto kuwa na wazazi, isipokuwa kama mtoto atanyimwa haki zake za kuwa na wazazi. Au, kama wazazi wataendelea kuzivunja haki za mtoto.
(d) Maoni ya mtoto, kama maoni hayo yametolewa kwa uhuru.
(e) Kwamba inafaa kuwaweka ndugu pamoja;
(f) Hitaji la kuwepo mwendelezo wa matunzo na udhibiti wa mtoto; na
( g) Jambo lolote ambalo mahakama itaona linafaa.
 
Kumuondoa Mtoto Kinyume cha Sheria
(i) Mtu yeyote atakuwa anatenda kosa, kama atamwondoa mtoto kutoka kwa mtu anayeishi naye kihalali, makazi yaliyoidhinishwa au taasisi, kinyume cha sheria.



SURA YA SABA
MATUNZO
Ni nani wanaweza kuomba kumtunza mtoto?
(i) Watu wafuatao wanaweza kuomba mahakamani amri ya kukimu mtoto:-
(a) Mzazi wa mtoto;
(b) Mlezi wa mtoto
(c) Mtoto mwenyewe, kwa kumtumia rafiki wa karibu;
(d) Ofisa wa Ustawi wa Jamii
(e) Ndugu wa mtoto.
(ii) Maombi ya kukimu mtoto yanaweza kufanywa dhidi ya mtu yeyote anayestahili kumtunza mtoto, au kwa madhumuni ya kuchangia kwa ajili ya ustawi na matunzo ya mtoto.

Amri ya kukimu mtoto dhidi ya anayesemekana ni baba mzazi wa mtoto
(i) Maombi ya amri ya kukimu mtoto yanaweza kufanywa mahakama ni dhidi ya baba anayesemekana kuwa baba mzazi wa mtoto.
46
Maombi ya kukimu yanaweza kufanywa na nani?
(a) Na Mama anayetarajia kujifungua wakati wowote kabla ya mtoto kuzaliwa;
(b) Na mzazi ambaye amri ya uzao imetolewa dhidi yake na mahakama.

Ni wakati gani maombi ya kukimu mtoto yanaweza kufanywa?
(c) Wakati wowote ndani ya miezi ishirini na nne (miaka miwili) baada ya kuzaliwa mtoto;
(d) Wakati wowote baada ya mtoto kuzaliwa, na baada ya kuthibitisha kwamba mwanamume anayesemekana kuwa ni baba wa kibaiolojia wa mtoto amelipa hela kwa ajili ya kumkimu mtoto ndani ya miezi ishirini na nne baada ya mtoto kuzaliwa.
(e) Wakati wowote ndani ya miezi ishirini na nne baada ya baba mzazi wa mtoto kurudi ndani ya Tanzania Bara, baada ya kuthibitika kwamba aliacha kuishi Tanzania kabla au baada ya mtoto kuzaliwa.
(ii) Mahakama itakataa kutoa amri ya kukimu mtoto chini ya kifungu cha (i) isipokuwa ikiridhika kwamba:
(a) Kuna sababu ya maana kuamini kwamba mwanamume anayesemekana ni baba wa mtoto, kweli ni baba wa mtoto, na kwamba maombi ya matunzo yamefanywa kwa nia njema wala si kwa lengo la kuogofya na kulazimisha malipo kwa nguvu; na
(b) Mwanamume anayesemekana kuwa ni baba wa mtoto ameombwa na mwombaji au mtu mwingine kwa niaba ya mwombaji kutoa matunzo ya mtoto naye amekataa au amepuuzia kutoa matunzo au ametoa kidogo.

Uamuzi kwa ajili ya Amri ya Kukimu Mtoto
(i) Mahakama itaangalia mambo yafuatayo inapotoa amri ya malipo ya matunzo:
(a) Kipato na utajiri wa wazazi wote wa mtoto au wa mtu ambaye kisheria anawajibika kutoa matunzo ya mtoto;
(b) Kama kipato cha mtu anayewajibika kutoa
matunzo ya mtoto kikididimia.
(c) Majukumu ya kifedha mtu aliyonayo kwa matunzo ya watoto wengine;
(d) Gharama za maisha za eneo ambapo mtoto anaishi; na
(e ) Haki za mtoto chini ya sheria hii.
48
(ii) Mtu yeyote ambaye anamlea mtoto anayehusika na amri ya kukimu mtoto anastahili kupokea na kusimamia amri ya mahakama ya kukimu mtoto.
(iii) Pale mzazi, mlezi au mtu yeyote anayemlea mtoto anapopoteza sifa za kuwa mtu anayefaa, mahakama iliyopo katika eneo analoishi mtoto inaweza kumteua mtu mwingine awe mlezi wa mtoto. Mtu huyu atasimamia amri ya kukimu mtoto na atatimiza majukumu yake kama vile aliteuliwa na mahakama tangu awali.

Muda wa Amri ya Kukimu Mtoto
(i) Amri ya kukimu mtoto iliyotolewa na mahakama itadumu mpaka mtoto anapofikisha umri wa miaka kumi na nane. Au itadumu hadi apate ajira inayompatia kipato. Au amekufa kabla ya kutimiza umri wa miaka kumi na nane.

Mwendelezo wa Amri ya Kukimu
(i) Mahakama inaweza kuendelea kutekeleza amri ya kukimu mtoto baada ya mtoto kutimiza umri wa miaka kumi na nane. Amri ya kukimu itaendelea kama mtoto bado anaendelea na masomo au mafunzo, licha ya muda wa ukomo kama ilivyoainishwa katika sheria hii.
(ii) Maombi chini ya fungu hili yanaweza kuletwa na mzazi wa mtoto, mtu yeyote anayemlea mtoto, au mtoto mwenyewe.
(iii) Mtu yeyote mwingine anaweza kupeleka maombi mahakami kutekeleza amri ya kukimu mtoto ndani ya siku arobaini na tano baada ya amri kutolewa au
kuwa tayari kwa utekelezaji.

Je, mzazi ambaye haishi na mtoto anaruhusiwa kumwona?
Mzazi ambaye haishi na mtoto ataruhusiwa kumtembelea mtoto. Jambo hili halizuiwi na amri ya kuthibitisha uzao, uangalizi, kumtembelea mtoto au ya kukimu mtoto iliyotolewa na mahakama dhidi yake.


FAHAMU KUHUSU MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGs)


SHULE INAYOTOA MICHEZO KAMA HII INAFAA KWA MZAZI NA MLEZI KUPELEKA MTOTO WAKE