Mara baada ya kutazama sheria
inasemaje kuhusu masuala ya Haki na Ustawi wa Mtoto, katika sehemu ya pili ya
mfululizo wa darasa juu ya Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, sasa naomba tutazame
sheria inasemaje katika masuala ya Kumtunza na Kumlinda Mtoto.
SURA YA TATU
KUMTUNZA NA KUMLINDA MTOTO
Maana ya Kumtunza na Kumlinda Mtoto
Ni mtoto yupi anastahili kulindwa?
Sheria hii inasema kwamba, mtoto
anahitaji huduma na ulinzi, iwapo mtoto huyu:
(a) Ni Yatima au ametelekezwa na
ndugu zake.
(b) Ameachwa au anatendewa vibaya na
mtu ambaye anamtunza na kumlea mtoto au na mlezi au wazazi.
(c) Ana mzazi au mlezi ambaye
hatekelezi majukumu yake kama anavyohitajika.
(d) Mtoto ni fukara.
(e) Yuko chini ya malezi ya mzazi au
mlezi ambaye hafai kumlea mtoto kwa sababu ni mhalifu au ulevi.
(f) Mtoto anazurura na hana makazi au
mahali pa kuishi.
(g) Ni ombaomba au anapokea misaada.
Au kama mtoto amekutwa mitaani, majumbani kwa lengo la kuomba au kupokea misaada.20
(h) Anaambatana na mtu ambaye anaomba
au anapokea misaada, iwe kwa kuhitaji au kutohitaji, kuimba, kucheza, kuigiza,
kutoa chochote kwa nia ya kuuza, au vinginevyo. Au amekutwa mitaani, majumbani kwa
lengo la kuomba au kupokea misaada.
(i) Yuko chini ya malezi ya mtu
fukara.
(j) Anapenda kuambatana na mtu mwenye
sifa ya uhalifu au ukahaba.
(k) Anaishi katika nyumba au sehemu
ya nyumba inayotumika na kahaba kwa lengo la kufanya ukahaba. Au anaishi katika
mazingira ambayo yanaweza kusababisha au yanachochea kutongozwa au kufanya ukahaba
au yanaweza kuathiri maadili ya mtoto.
Mtu asiyefaa Mtu asiyefaa kumlea
na kumlinda mtoto ana sifa gani?
(i) Ni mtu ambaye amefanya kosa au amejaribu
kufanya kosa kuhusiana na sheria inayozuia kusafirisha binadamu.
(a) Amekutwa akifanya jambo linaloashiria
kuwa amekuwa anaomba au ameshaomba au anaombaomba kwa nia ya kutongoza
kusikoendana na maadili.
(b) Ana umri chini ya miaka ishirini
na moja na amehusika katika kutenda kosa la jinai.
(c) Yuko katika mazingira hatari
kimwili na kimaadili. Kwa mfano, mtu anayefanya kazi akiwa uchi, mahali pa
kutengenezea pombe, au mahali watu wazima wanatumia lugha chafu.
2(d) Yuko chini ya matunzo ya mtu mlemavu ambaye uwezo wake unamzuia kutimiza majukumu yake kama mlezi.
(e) Yuko katika mazingira yoyote
ambayo Kamishna anaweza kuamua.
(f) Mtu ambaye ni mmiliki au mkazi
anayeendesha au ni msimamizi wa disko, baa au klabu ya usiku, haruhusiwi
kumruhusu mtoto kuingia katika jumba hilo.
(g) Mtu haruhusiwi kumuingiza mtoto
mahali popote ambapo inafanyika shughuli ya kuuza sigara, pombe, au kilevi chochote,
madawa au kitu chochote kinachoweza kumlevya mtoto.
(h) Mtu anayevunja sheria katika
fungu hili, anatenda kosa. Akipatikana na hatia, atawajibika kulipa faini si
chini ya shilingi milioni moja lakini isiyozidi shilingi milioni tano au
kifungo kwa muda usiozidi miezi kumi na mbili, au yote kwa pamoja.
Amri ya muda ya matunzo
Mahakama inaweza kutoa amri ya
matunzo au amri ya matunzo ya muda baada ya maombi kupelekwa na Ofisa wa Ustawi
wa Jamii kwa faida ya mtoto.
Amri ya matunzo au amri ya muda ya
matunzo itamuondoa mtoto kutoka mahali alipokuwa akiteseka, au ambapo angeweza
kupata madhara makubwa na kuhamisha haki za mzazi kwa Ofisa wa Ustawi wa Jamii.
23
Ofisa wa Ustawi wa Jamii atamtunza
mtoto na kuamua mahali panapofaa mtoto kuishi ambapo panaweza kuwa:
(a) Makazi yaliyoidhinishwa.
(b) Mtu anayefaa.
(c) Mzazi, mlezi aliyethibitishwa
kulingana na kanuni za matunzo ya malezi zilizotengenezwa chini ya sheria hii.
(d) Nyumbani kwa mzazi, mlezi au
ndugu. Muda wa ukomo wa amri ya malezi utakuwa miaka mitatu, au mpaka mtoto
afikishe umri wa miaka kumi na nane. Hii itategemea ni muda upi utaanza
kukamilika.
24
Mahakama inaweza kutoa amri ya ziada
kwamba mzazi, mlezi au mtu yeyote atawajibika kulipa gharama za matunzo ya
mtoto.
Mahakama itamteua na kuidhinisha
meneja au mlezi wa taasisi au makazi yaliyoidhinishwa, kama mtu anayefaa kukabidhiwa
kumlea mtoto baada ya Kamishna kutangaza kwenye gazeti la serikali.
Amri ya muda ya malezi itatolewa tu
pale ambapo mtoto anapokuwa katika mateso au anaweza kupata mateso makubwa kama
ilivyoainishwa katika Sheria hii.
Amri ya Usimamizi ya Mahakama
(i) Ofisa Ustawi wa Jamii, ataomba
mahakama kutoa amri ya usimamizi au amri ya muda ya usimamizi.
Nia ya amri ya usimamizi ni nini ?
(ii) Amri ya usimamizi au amri ya
muda ya usimamizi itakuwa na nia ya kumweka mtoto chini ya matunzo ya wazazi,
walezi au ndugu. Madhumuni yake ni kuzuia mateso makubwa anayopata mtoto akiwa katika
makazi ya familia.
(iii) Amri ya usimamizi au amri ya
muda ya usimamizi itamweka mtoto chini ya usimamizi wa Ofisa wa Ustawi wa Jamii
au mtu yeyote anayefaa. Mtu huyo atakuwa katika jamii alimo mtoto wakati akiwa
chini ya malezi ya mzazi, mlezi au ndugu.
25
Amri ya usimamizi itadumu kwa muda
gani ?
(iv) Muda wa ukomo wa amri ya
usimamizi utakuwa mwaka mmoja au mpaka mtoto atakapofikisha umri wa miaka kumi
na nane. Ofisa wa Ustawi wa Jamii, anaweza kwa ridhaa yake, akatoa maombi kuhusu
kuongeza au kupunguza muda wa amri ya usimamizi.
(v) Kuongezwa kwa muda wa amri ya
usimamizi kutahitaji taarifa ya maandishi ya Ofisa Ustawi wa Jamii.
(vi) Amri ya usimamizi itahitaji mtu
anayeishi na mtoto:
(a) Kumtaarifu msimamizi mabadiliko
yoyote ya anuani; na
(b) Kumruhusu msimamizi kumtembelea
mtoto nyumbani kwa mlezi.
(vii) Maombi kwa ajili ya amri ya
kumpokea mtoto kwenye makazi yaliyoidhinishwa au taasisi yatakuwa na taarifa
zinazohusu:
(a) Jina, umri na anuani ya mtoto;
(b) Jinsia ya mtoto;
(c) Jina la mzazi, kama linafahamika;
(d) Utaifa;
(e) Elimu ya mtoto;
(f) Taarifa ya daktari kuhusu afya ya
mtoto;
(g) Mahali alipozaliwa mtoto, kama
panafahamika;
(h) Kabila; na
(i) Dini aliyozaliwa nayo.
(viii) Maombi yaliyofanywa chini ya
fungu hili yatazingatia:
(a) Ustawi wa mtoto;
(b) Taarifa ya uchunguzi wa Ustawi wa
Jamii; na
(c) Familia mbadala.
Wajibu wa Ofisa wa Ustawi wa Jamii Ustawi
wa Jamii unamsaidiaje mtoto kuhusu malezi na usimamizi?
(i) Wajibu wa Ofisa wa Ustawi wa
Jamii kuhusu amri za malezi na usimamizi wa mtoto ni:
(a) Kutoa ushauri na mawaidha kwa
mtoto na familia.
(b) Kukumbusha mara kwa mara kuhusu
mipango ya baadaye ya mtoto kwa kushauriana na mtoto na wazazi au mlezi.
(c) Kupeleka maombi mahakamani ili
kusitisha amri au kubadili amri kama kuna ulazima; na
(d) Kuchukua hatua za lazima ili
kuhakikisha kuwa mtoto hawezi kudhurika.
Kumtembelea nyumbani
(i) Ofisa wa Ustawi wa Jamii
ataruhusiwa na wazazi, walezi au ndugu wa mtoto kumtembelea mtoto kwenye makazi
ya familia, au katika makazi yaliyoidhinishwa au taasisi, kwa vyovyote inavyowezekana.
Sheria ya Jumla juu ya Amri
(i) Mtoto anayekiuka amri ya mahakama
na kukimbia anaweza kukamatwa na polisi na kurudishwa mahali pa malezi bila
kibali cha kukamata. Kibali hiki kinatoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Ofisa Mtendaji
wa Kata, au Ofisa wa Ustawi wa Jami .
(ii) Pale mtoto anapokuwa amekimbia,
na mtu anayefaa wa kumlea hayuko tayari kumlea, mahakama inaweza kutoa amri
nyingine ya kumweka mtoto chini ya malezi ya shule iliyoidhinishwa.
Kuondoa Amri
(i) Amri ya matunzo au usimamizi
inaweza kuondolewa na mahakama kwa ajili ya ustawi wa mtoto, baada ya maombi
kupelekwa na:
(a) Mtoto, kupitia rafiki wa karibu;
yaani, ndugu au mtu anayeaminiwa na mtoto.
(b) Ofisa wa Ustawi wa Jamii;
(c) Ofisa wa Polisi;
(d) Mzazi, mlezi au ndugu wa mtoto;
au
( e) Mtu yeyote mwenye majukumu ya
mzazi.
Mtoto anakuwa na haki Wazazi
Wanapotengana Mtoto atakuwa na haki gani wazazi wake wakitengana?
(i) Kwa kuzingatia Sheria ya Ndoa,
wazazi wanapotengana au wanapotalikiana, mtoto atakuwa na haki ya:
(a) Kupata matunzo na elimu yenye
hadhi kama ilivyokuwa kabla wazazi hawajatengana
au hawajatalikiana;
(b) Kuishi na mzazi ambaye, kwa maoni
ya mahakama, ana uwezo wa kumlea na kumpatia matunzo kwa kiwango kinachostahili
kwa ustawi wa mtoto: na
(c) Kumtembelea na kukaa na mzazi
mwingine kila anapohitaji, isipokuwa kama mpango huo utaathiri ratiba ya shule
au mafunzo kwa mtoto.
(ii) Kwa ajili ya kudumisha furaha na
amani ya mtoto, mategemeo ni kwamba mtoto mwenye umri chini ya miaka saba
ataishi na mama. Hata hivyo, jambo hilo linaweza kupingwa. Maamuzi
yatakayofanywa kwa kuzingatia pingamizi kuwa mtoto asikae na mama, mahakama itaangalia
uwezekano wa kumsumbua mtoto katika maisha yake kwa kubadili makazi.
No comments:
Post a Comment