Kila ifikapo tarehe 16 Juni, Afrika na Ulimwengu kwa ujumla unaadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika, siku ambayo inatukumbusha ukatili na unyama mkubwa aliofanyiwa mtoto wa Afrka huko katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini.
Siku hii ilipitishwa rasmi mwaka 1990 na Umoja wa
Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao kwa sasa unafahamika kama Umoja wa Afrika (AU).
Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU) ulipitisha
azimio la kuwakumbuka watoto waliouawa kikatili mnamo tarehe 16 Juni 1976,
wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo
haki ya kupata elimu bora, ambapo walipinga matumizi ya lugha ya Afrikaan
katika kujifunza na kufundishia.
Kama kweli tunayo nia ya dhati ya kuadhimisha
siku hii, basi moja ya jambo la msingi ambalo tunapaswa kulifanya, ni Kumlinda
Mtoto wa Kitanzania.
Mtoto wa Kitanzania amekuwa akikumbwa na changamoto
nyingi ambazo zinamfanya asifurahie ile hali ya kuwa mtoto, na badala yake
kuuchukia utoto wake ambao umejaa manyanyaso na ukatili wa kupindukia.
Zifuatazo ni sababu ambazo zinamfanya Mtoto wa
Kitanzania asifurahie hali yake ya utoto. sababu hizi zinatokana na uzoefu
wangu mimi mwandishi katika kuishi na watoto, maana napenda sana kuwa karibu na
watoto, vilevile nimebahatika kuishi sehumu za mjini na vijijini, hasa katika
yale maeneo ambayo yanafahamika sana kama vinara wa unyanyasaji watoto.
1.
Utumikishaji Watoto (Kazi ngumu kwa watoto).
Licha ya jitihada kubwa za serikali katika
kutokomeza utumikishwaji wa watoto katika umri mdogo, bado katika baadhi ya
maeneo hapa nchini watoto wamekuwa wakitumikishwa. Watoto hawa wamekuwa
wakiajiriwa kufanya kazi za ndani, maarufu kwa jina la ‘beki tatu’ hapa nchini
Tanzania. Wengi wa watoto hawa ni wadogo sana ambao ukitazama umri wao
wanastahili kuwa shule wakipata haki yao ya msingi yakupata Elimu.
Mbali na kazi za ndani ambazo mara nyingi ni kwa
watoto wa kike, kwa upande wa watoto wa kiume, wao wamekuwa wakiajiriwa kufanya
biashara ya uchuuzi katika maeneo mbalimbali ya majiji na miji, ikiwemo
kutembeza biashara hizo (karanga, ndizi, vinywaji baridi, n.k) katika maeneo ya
stendi (vituo vya magari), na mbaya zaidi wengine hutembeza bishara hizo katika
nyumba za starehe, yaani nyumba za kulala wageni (Guest House) na kwenye Bar.
2.
Ndoa za Utotoni.
Changamoto nyingine inayomkumba Mtoto wa
Kitanzania ni ndoa za utotoni. Watoto wa kike wamekuwa wakilazimishwa kuolewa
katika umri mdogo hasa katika jamii za wakulima na wafugaji hapa nchini.
Binafsi natokea katika moja ya jamii ambayo inafanya vitendo hivi, na mara
kadhaa nimeshuhudia kwa macho yangu vikifanyika.
Watoto wengi wa kike wanapohitimu Darasa la Saba,
na matokeo yao kuonesha kuwa hawajachaguliwa kujiunga na Elimu ya Sekondari,
basi wazazi ama walezi wa watoto hao huona kitu pekee cha kumfanyia mtoto wa
kike ambaye ameshindwa kuendelea na Elimu ya Sekondari, ni kumuozesha. Wengine
huwaozesha watoto wao kwa kisingizio cha umaskini, wakidai kuwa endapo binti
yao ataolewa wao kama familia watapata mali, na binti yao ataondoka nyumbani,
na hivyo kupunguza mzigo kwa familia.
3.
Ukeketaji
Ukeketaji ni changamoto nyingine inayomkumba
Mtoto wa Kitanzania hapa nchini. Jamii nyingi za Wafugaji zimeendelea kufanya
kitendo hichi cha kikatili kwa mtoto wa kike. Licha ya jitihada kubwa za
kutokomeza suala la ukeketaji nchini, zinazofanywa na Serikali pamoja na
Mashirika mbalimbali kama Plan Tanzania, Children’s Dignity Forum (CDF), na
Save the Children (kutaja kwa uchache), bado vitendo vya ukeketaji vimeendelea
kufanyika kwa siri katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Mtoto wa Kike
ameendelea kufanyiwa unyama huu ambao umfanya ahisi maumivu makubwa nay a kutisha,
maana wahusika wa vitendo hivi, yaani Nghariba, uwafanyia unyama huu watoto
hawa kwa kuwakata sehemu zao pasipo ganzi.
4.
Adhabu za Kinyama kwa Watoto (Fimbo, Makofi, n.k)
Mtoto wa Kitanzania ameendelea kupokea adhabu za
kinyama ambazo huambatana na kuchapwa fimbo kali na nyingi, kupigwa makofi,
kuchomwa moto baadhi ya viungo vyake kama viganja vya mikono, n.k. Vitendo hivi
hakika vinaumiza sana, na kuna muda nafikiria wanofanya vitendo hivi huwa
wanafikiria nini au ni pepo gani huwa amewashukia na wao kufanya ukatili wa
namna hii.
Kesi za mtoto kuunguzwa moto kwa kosa la kupoteza
hela, kuiba hela, na hata kukwapua mboga chunguni (kukomba mboga) zimekuwa za
kawaida sana masikioni mwa Watanzania kiasi cha kuanza kuzoeleka sasa. Hakika
hili sio jambo jema hata kidogo, chonde chonde, nawaomba tuungane kupinga
ukatili huu.
5.
Mazingira Hatarishi kwa Watoto Mashuleni.
Huenda nisieleweke vyema katika jambo hili,
lakini baadhi ya mazingira ya shule zetu nchini Tanzania sio rafiki kwa watoto
wadogo. Miundombinu katika baadhi ya shule zetu bado inayaweka hatarini maisha
ya mtoto. Baadhi ya shule zimeendelea kutumia vyoo vya matundu ambavyo ni
hatari sana kwa watoto wadogo hasa wale wa darasa la kwanza na chekechea
(awali). Watoto hawa wanaweza kutumbukia katika matundu haya, na hivyo
kupelekea kupata vilema vya maisha na hata kupoteza uhai.
Ombi Langu kwa Watanzania Wote.
Nawaomba tuhakikishe tunafanya kila liwezekanalo,
kila lililopo katika uwezo wetu kuhakikisha tunawalinda watoto, hasa watoto wa
vijijini ambao hawana mtu wa kuwasemea. Watoto wengi wamekuwa wakifanyiwa
vitendo vya ukatili bila kupata msaada wowote kutoka kwa jamii. Kama Watanzania
nawaomba tufahamu kuwa jukumu la kumlinda mtoto ni jukumu la kila mmoja wetu,
tukumbuke kuwa nasisi tulikuwa watoto, hivyo tujiulize kama nasisi tungefanyiwa
vitendo vya kikatili kama tunavyowafanyia wao hii leo tungefika hapa tulipo?.
Pia tuhakikishe tunashirikiana na Serikali katika
kutokomeza Kazi ngumu na Ajira za Utotoni kwa kutoa elimu juu ya athari ya
tabia hiyo, na kama watu wataendelea na tabia hii basi tuwaripoti kwa vyombo
vinavyohusika kwa hatua za kisheria.
Kuhusu ndoa za utotoni, nashauri watanzania
wenzangu ambao wanaendelea kuwaozesha watoto wao katika umri mdogo kuacha mara
moja, maana kitendo hiki ni kinyume kabisa na haki za mtoto. Tukumbuke kuwa
ndoa za utotoni zinaweza kukatisha maisha ya mtoto pale atakapopata ujauzito na
kwakuwa umri wake ni mdogo anaweza kupata matatizo ya uzazi ambayo yanaweza
kumsababishia kifo. Vilevile kwa kumuozesha binti akiwa angali mdogo tunamnyima
haki yake ya msingi ya kupata elimu, ikiwa ni pamoja na kumnyima fursa ya
kutimiza malengo yake. Chonde chonde tuache tabia hii mara moja.
Kuhusu suala la ukeketaji kwa watoto wa kike,
nawaomaba wale wote wanaoendelea kufanya kitendo hiki cha kinyama kuacha mara
moja. Pia jamii tushirikiane katika kutokomeza janga hili. Jamii inapaswa kutoa
taarifa kwenye mamlaka zinazo husika punde ionapo matukio haya yakifanyika.
Tukumbuke kuwa mabadiliko uanza na mtu mmoja mmoja (wewe). Usiogope kuripoti
matukio haya kisa jamii yako haina utamaduni wa kufanya hivyo. Kwa pamoja
tutatokomeza Ukeketaji.
Kuhusu adhabu za kinyama kwa watoto wetu, naomba
watanzania wote tuache mara moja kutoa adhabu ambazo zinahatarisha ustawi wa
mtoto. Sikatai kuwa adhabu zisitolewe kabisa, lakini ninachokataa ni adhabu za
kikatili. Tuangalie njia mbadala za kutoa adhabu, mathalani, kuliko kumchapa
mtoto, wazazi wanaweza kumpa adhabu ya kutokwenda kucheza na wenzake mtoto
aliyefanya kosa kwa siku husika. Jambo la muhimu nashauri wazi na walezi kuwa
karibu sana na watoto, yaani kujenga urafiki nao ili iwasaidie kujua watoto wao
wanataka nini na wana tabia zipi ambazo zinapaswa kurekebiswa kwa wakati huo.
Kuhusu Mazingira Hatarishi kwa Watoto Mashuleni,
nashauri serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuboresha miundombinu
ambayo inaonekana kuhatarisha maisha ya watoto wetu. N I lazima tuhakikishe
mazingira yetu yote yanakuwa salama kwaajili ya watoto wetu kustawi na kuishi.
TUWALINDE WATOTO.
No comments:
Post a Comment