Mara baada ya kutazama Utangulizi wa
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa darasa
juu ya sheria hii, sasa ni wakati muafaka wa kuanza kuichambua sheria yenyewe.
Katika sehemu hii ya pili tutaangalia HAKI NA USTAWI WA MTOTO.
SURA YA PILI
8
HAKI NA USTAWI WA MTOTO
Mtoto ni nani?
Mtoto ni mtu aliye na umri chini ya
miaka kumi na nane.
Ustawi wa mtoto; yaani, furaha na amani kwa mtoto itapewa
kipaumbele katika kutathmini mambo yote yanayomhusu mtoto, yawe yamefanywa na
taasisi ya Ustawi wa Jamii ya serikali au binafsi , mahakama au vyombo vya
utawala.
Haki za Mtoto
1. Haki ya Kutokutengwa
Mtoto atakuwa na haki ya kuishi huru
bila kuwapo na namna yoyote ya kutengwa; yaani, kuonekana kuwa hastahili
kujumuika na wenzake katika kundi. Mtu yoyote haruhusiwi kumtenga mtoto kwa
sababu za:
- Jinsia, rangi, umri au dini.
- Mtu hatakiwi kumtenga mtoto kwa sababu anaongea lugha tofauti.
- Mtoto hatakiwi kutengwa kwa sababu ametoa maoni tofauti ya kisiasa.9
- Mtoto hatakiwi kutengwa kwa sababu ni mlemavu au kwa hali yake ya afya.
- Mtoto hatakiwi kutengwa kwa sababu ya kabila lake au mila zake.
- Mtoto hatakiwi kutengwa kwa sababu anatoka kijijini au mjini.
- Mtoto hatakiwi kutengwa kwa sababu ya hali yake ya kijamii na kiuchumi, au
- Kwa kuwa ni mkimbizi au hali yoyote nyingine.
10
2. Haki ya Jina na Utaifa
Mtoto ana haki ya kujua jina lake,
utaifa, na wazazi wake waliomzaa na ukoo wa familia yake. Mtu yeyote haruhusiwi
kumnyima mtoto haki ya kujua jina lake, utaifa, na kujua wazazi wake waliomzaa
na wengine katika ukoo wa wazazi wake.
11
3. Haki ya Kuishi na Wazazi au Walezi
Mtoto ana haki ya kuishi na wazazi au
walezi wake. Mtu yoyote haruhusiwi kumnyima mtoto haki ya kuishi na wazazi,
walezi au familia yake. Pia, ni haki ya mtoto kukua katika malezi na mazingira
ya amani. Isipokuwa ikiamriwa na mahakama kwamba kuishi na wazazi au familia
kunaweza:
(a) Kusababisha madhara makubwa kwa
mtoto, hasa pale ambapo mtoto ananyanyaswa.
(b) Kumweka mtoto katika mazingira ya
kutendewa vibaya;
(c) Sio vema kwa ajili ya ustawi wa
mtoto, yaani, mahali ambapo mtoto haishi kwa furaha na amani. Kwa kufuatana na
sheria na taratibu zinazotumika, Mamlaka yenye uwezo, mfano, Serikali ya Mtaa, au
mahakama, inaweza kuamua kwamba mtoto atenganishwe na wazazi, kwa sababu ya
ustawi wake. Ikitokea hivyo, mtoto lazima apewe malezi mbadala.
4. Wajibu wa kumtunza mtoto
Ni wajibu wa mzazi, mlezi au mtu
yeyote mwenye kumlea mtoto kutoa matunzo kwa mtoto. Wajibu huu hasa unampatia
mtoto haki ya:
12
(a) Chakula;
(b) Malazi;
(c) Mavazi;
(d) Dawa pamoja na chanjo;
(e) Elimu na maelekezo au mafunzo;
(f) Uhuru; na
(g) Haki ya kucheza na kupumzika.
5. Haki ya Kupata Huduma
Mtu yeyote haruhusiwi kumnyima mtoto
haki ya kupata elimu, chanjo, chakula, mavazi, malazi, huduma ya afya na dawa
au kitu chochote kinachohitajika kwa ajili ya
maendeleo ya mtoto. Mtu yeyote haruhusiwi
kumkatalia mtoto huduma ya dawa kwa sababu ya dini au imani yoyote ile.
6. Haki ya Kushiriki Michezo na
Shughuli za Kiutamaduni
Mtu yeyote haruhusiwi kumnyima mtoto
haki ya kushiriki katika michezo, au shughuli njema za kiutamaduni na kisanii
au za starehe. Hata hivyo, ikiwa kwa maoni ya mzazi, mlezi au ndugu, kwamba
kushiriki huko kutakuwa na madhara, au shughuli hizo haziendelezi ustawi wa mtoto,
haki hiyo inaweza isitolewe. Mtu yeyote haruhusiwi kumtendea mtoto mwenye ulemavu
tendo lolote kwa namna isiyo ya heshima.
Watoto wenye ulemavu wa aina yoyote
ile wanastahili msaada na upendo.
7. Haki ya Huduma ya pekee kwa
Mlemavu
Mtoto mwenye ulemavu anastahili
kupewa huduma ya pekee. Huduma hizi ni pamoja na: kutibiwa, kupewa nyenzo
stahili kwa ajili ya kurekebisha ulemavu wake. Kwa mfano, viti na baiskeli za
walemavu wa viungo, fimbo kwa kipofu au hati za alama kwa bubu. Mlemavu ana
haki ya kupewa nafasi sawa katika elimu na mafunzo pale inapowezekana, ili kuendeleza
vipaji vyake na uwezo wa kujitegemea.
14
8. Wajibu na Jukumu la Mzazi
Mtoto atakuwa na haki ya kuishi, kwa
hadhi, heshima, uhuru, afya, kupumzika, na kupatiwa elimu na malazi kutoka kwa
wazazi. Haki ya kupumzika na uhuru kwa mtoto vitategemea maelekezo na uwezo wa
wazazi, walezi au ndugu.
Kila mzazi ana wajibu na majukumu kwa
mtoto. Wajibu na majukumu hayo yatatekelezwa, yawe yamewekwa na sheria au
vinginevyo.
Yanahusisha wajibu wa:
(a) Kumlinda mtoto dhidi ya
kutelekezwa, kutengwa, kufanyiwa vurugu, kunyanyaswa, kutumiwa vibaya, na kuwa
katika mazingira mabaya kimwili na kimaadili.
(b) Kutoa maelekezo, uangalizi,
msaada, na hifadhi kwa ajili ya mtoto, na uhakika wa maisha na maendeleo ya
mtoto.
(c) Kuhakikisha kuwa wazazi
wanapokuwa mbali na mtoto, mtoto atapata uangalizi kutoka kwa mtu mwenye uwezo
wa kutimiza majukumu hayo.
Wajibu na majukumu haya yanasitishwa
wakati wazazi wanapotoa wajibu na majukumu hayo kwa mtu mwingine. Kutoa
majukumu kutoka kwa mzazi kwenda kwa mtu mwingine kunafanywa kulingana na
sheria iliyoandikwa au kwa mpango wa mila na desturi.
15
Iwapo wazazi waliomzaa mtoto
wamefariki, wajibu wa wazazi utahamia kwa ndugu wa mzazi wa kiume au wa kike au
mlezi. Watapewa wajibu na majukumu hayo kwa amri ya mahakama, au mpango wowote
utakaowekwa kimila.
9. Haki kwa Mali za Wazazi
Mtu haruhusiwi kumnyima mtoto
kumiliki na kutumia mali ya urithi kutoka kwa mzazi.
10. Haki ya Kutoa Maoni
Mtoto atakuwa na haki ya kutoa maoni.
Hakuna mtu anayeruhusiwa kumnyima mtoto mwenye uwezo wa kutoa maoni haki ya
kueleza maoni, kusikilizwa na kushiriki katika kufanya maamuzi yatakayoathiri
ustawi wake.
16
11. Ajira yenye Madhara
Mtu yeyote haruhusiwi kumuajiri mtoto
katika shughuli yoyote inayoweza kuwa na madhara katika maendeleo ya afya,
elimu, akili, mwili na maadili yake. Kwa mfano, kazi
katika viwanda vya kemikali inaleta
athari kwa afya ya mtoto. Kazi ya mashambani au machimboni inayozuia mtoto
kwenda shule inaathiri elimu, akili na mwili wake.
Kazi ya ukahaba inaathiri maadili ya
mtoto.
12. Kulinda Mtoto Asiteswe na
Kudhalilishwa
Mtu yeyote hataruhusiwa kumfanya
mtoto apate mateso, au adhabu ya kikatili, ya kinyama au afanyiwe matendo yenye
kumshushia hadhi. Hii ni pamoja na desturi zozote za mila zenye kudhalilisha
utu wa mtoto au zinazosababisha athari za maumivu ya mwili au akili ya mtoto.
Kwa mfano, kukeketa wasichana ni kudhuru vibaya mwili, akili na hisia za mtoto
wa kike. Pia, ni kitendo kinachomdhalilisha.
Hakuna adhabu kwa mtoto inayokubalika
ambayo imekithiri kimatendo au kwa kiwango kulingana na umri, hali ya mwili na
akili yake. Hakuna adhabu inayokubalika
kwa ajili ya umri mdogo wa mtoto au
vinginevyo kwa sababu mtoto hawezi kuelewa nia ya adhabu hiyo.
Tendo lenye kudhalilisha, kama maneno hayo yalivyotumika katika
fungu hili una maana ya tendo lililofanywa kwa mtoto kwa nia ya kudhalilisha au
kumshushia hadhi yake. Kwa mfano, kuchapa mtoto mbele ya wenzake au mbele ya
umma wa watu ni tendo lenye nia ya kumdhalilisha mtoto.
Je, adhabu ya kukiuka sheria ya haki
za mtoto ni ipi?
Mtu anayevunja sheria kama
ilivyoainishwa katika sehemu hii, anatenda kosa. Baada ya kutiwa hatiani kwa
kutenda kosa hilo, atawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo
kwa muda usiozidi miezi sita au vyote kwa pamoja.
18
Wajibu wa Jumla wa Mtoto
Mtoto ana haki, lakini pia ana wajibu.
Je, wajibu wa mtoto ni upi?
Pamoja na haki za kulinda ustawi wa
mtoto, mtoto atakuwa na wajibu na jukumu la:
(a) Kufanya kazi kwa ajili ya
mshikamano wa familia.
(b) Kuwaheshimu wazazi, walezi,
wakubwa wake na watu wazima muda wote na atawasaidia pale inapohitajika.
(c) Kuhudumia jamii yake na taifa
lake kwa uwezo wake wote kimwili na kiakili kadiri ya umri na uwezo wake.
(d) Kutunza na kuimarisha mshikamano
wa jamii na Taifa; na
(e) Kutunza na kuimarisha mambo mema
katika utamaduni wa jamii na Taifa kwa ujumla katika uhusiano na wanajamii au
taifa.
Bila shaka sasa tumeelewa juu ya
masuala yote yanayohusu HAKI NA USTAWI WA MTOTO kama yanavyoelezwa kwenye
sheria hii. Ni mategemeo yangu kuwa kila mtu aliyepata fursa ya kusoma makala
hii atahakikisha anazingatia matakwa ya sheria hii, na hakuna yeyote
atakayeshiriki kitendo chochote kitakachoashiria ukatili dhidi ya mtoto.
No comments:
Post a Comment