Showing posts with label The SDGs. Show all posts
Showing posts with label The SDGs. Show all posts

Friday, June 29, 2018

TUTEKELEZE MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGs) [SEHEMU YA TATU]

Mara baada ya kuona lengo namba 6 hadi namba 10 katika makala iliyopita. Sasa tutazame lengo namba 11 hadi namba 17. Je unafahamu lengo namba 11 linahusu nini? vipi kuhusu lengo namba 12, 13,14, 15, 16, na 17?, Utekelezaji wake ukoje? Basi karibu uungane nami katika sehemu ya tatu ya mfululizo huu wa darasa kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
 
 
Miji na Jamii Endelevu

Lengo hili linalenga kuweka miji, majiji, na makazi ya watu kuwa jumuishi, salama, imara na endelevu. Linasisitiza serikali na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha zinazuia ujenzi holela kwa kuweka mipango miji na kuhakikisha zinatenga maeneo maalumu kwaajili ya ujenzi wa maeneo ya kijamii kama viwanja vya mipira, masoko, na nyumba za serikali.

Vile vile linalenga kuzuia ujenzi wa makazi kwenye maeneo hatarishi, na kwa yale ambayo tayari watu washajenga basi wapewe mahali salama kwa ajili ya makazi. Linasisitiza pia ujenzi wa miundombinu ya usafiri kwa umma kuzingatia watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu, wazee na watoto.

Linahimiza pia kuweka mipango mikakati ya kuendeleza huduma za msingi vijijini ili kuwepo uwiano kati ya Miji na Vijiji. Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Serikali Kuu zina wajibu wakutambua urithi wa asili na utamaduni na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo mfano; mapango, wanyama, majengo ya kale, nakadhalika. 

Nchini Tanzania lengo hili bado halijapewa kipaumbele kwani maeneo mengi ya nchi yamejengwa pasipo kufuata utaratibu wa mipango miji, nyumba zimebanana kiasi cha kutoruhusu hata barabara za mitaa kupita na kufanya utoaji huduma muhimu kama zima moto kushindwa kuwafikia wananchi kwa ufanisi pindi majanga ya moto yanapotokea. Kwa uzoefu wangu na kwa maono yangu binafsi, ni mji wa Dodoma pekee ambao umejitahidi kupangiliwa vizuri ukilinganisha na miji mingine.
Lakini pia suala la uwiano wa huduma za kijamii kati ya sehemu ya mijini na vijijini bado limeendelea kuwa changamoto kwani hakuna uwiano sawa wa upatikanaji wa huduma hizo.


Matumizi na Uzalishaji wenye Uwajibikaji

Lengo hili linalenga kuhakikisha kunakuwepo na mifumo endelevu ya utumiaji na uzalishaji wa rasilimali. Linasisitiza pia juu ya kupunguza kiasi kikubwa cha taka kupitia mifumo endelevu ya kuzuia, kupunguza, na kuzichakata tena kwa matumizi mengine. Suala la kupunguza upotevu wa chakula unaosababishwa na njia mbaya za uzalishaji na usambazaji, ikiwa ni pamoja na hasara baada ya mavuno pia limepewa msisitizo wa kutosha.

Linasisitiza pia juu ya kuhakikisha manunuzi ya umma yanakuwa endelevu kulingana na sera na vipaumbele vya kitaifa. Suala la uanzishwaji wa zana za kusimamia matokeo chanya ya maendeleo endelevu kwaajili ya utalii ambao unazalisha ajira na kuhamasisha utamaduni na bidhaa za ndani pia limepewa uzito wake.

Katika kutekeleza lengo hili, nchi ya Tanzania imefaulu kwa kiasi chake hasa katika kusimamia rasilimali zake kama madini. Kumetungwa sheria zinazosimamia uzalishaji wa madinni ambao una manufaa kwa taifa. Suala la uzuiaji taka pia halijaachwa nyuma, jitihada mbalimbali zimekuwa zikioneshwa na serikali katika kupambana na uzalishaji taka nchini.


Kuchukua Hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabia Nchi

Lengo hili linalenga kuhakikisha nchi zote duniani zinachukua hatua za haraka kupambana na mabadiliko ya hali ya nchi pamoja na athari zake. Limekusudia kuimarisha uwezo wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na majanga yote katika nchi zote za ulimwengu.
Linalenga pia kuboresha elimu na kuhamasisha watu pamoja na taasisi mbalimbali kupunguza kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na njia za kukabiliana na mabadiliko hayo kwa kutoa tahadhari kabla ya kutokea.

Linadhamiria pia kukuza utaratibu wa kuongeza uwezo wa mipango na usimamizi wa hali ya hewa inayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi ambazo zinaendelea kukua na nchi ndogo za visiwa vinavyoendelea, huku msisitizo ukiwa kwa kundi la wanawake, vijana na jamii zilizotengwa.
Suala la kuingiza kwenye sera za nchi na mipango mbalimbali hatua zote zinazotakiwa kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi pia linapewa msisitizo katika lengo hili.

Nchini Tanzania hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwa ni pamoja na kuhimiza zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya nchi kama moja ya hatua katika kutekeleza lengo hili.

Licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi, nguvu zaidi bado zinahitajika ikiwa pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi dhidi ya athari ya ukataji miti ovyo ambayo ni moja ya sababu zinazopelekea mabadiliko ya tabia ya nchi kama ukame kutokea.


Kuendeleza Uhai katika Maji

Lengo hili linahimiza juu ya kuhifadhi na kutumia kwa njia endelevu malighafi za baharini kwa ajili ya maendeleo endelevu. Limedhamiria kufikia mwaka 2025, kunakuwa na matokeo chanya katika kuzuia na kupunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa kila aina unaofanywa baharini ikiwa ni matokeo ya shughuli mbalimbali za binadamu zinazoendelea kwenye fukwe za bahari.

Lina lenga pia kufikia mwaka 2020, kuwe na matokeo chanya katika kuhifadhi angalau asilimia 10 ya maeneo ya pwani na bahari, kulingana na sheria za kitaifa na kimataifa juu ya usimamizi wa bahari. Usimamizi wa shughuli za uvuvi na kuzuia uvuvi haramu pia ni miongoni mwa mambo yanayopewa uzito katika lengo hili la 14.

Nchini Tanzania kumekuwa na jihada za kulizisha katika kutekeleza lengo hili. Kumetungwa sheria mbalimbali za kulinda, kuifadhi, na kuendeleza viumbe vya baharini na ziwani. Uvuvi haramu umekuwa ukipigwa vita, huku hatua stahiki zikichukuliwa ikiwa ni pamoja na uchomaji nyavu zisizostahili.

Licha ya matokeo chanya katika kutekeleza lengo hili, changamoto mbalimbali zimeendelea kuwepo ikiwa ni pamoja na shughuli zenye kuhatarisha uhai wa viumbe vya baharini kwenye maeneo ya ufukwe, uvuvi wa kutumia sumu, na kadhalika.


Kulinda Uhai katika Ardhi

Lengo hili linalenga kulinda uhai katika ardhi na baionuwai. Linasisitiza juu ya kulinda na kurejesha katika hali ya awali mifumo ya mazingira ya nchi kavu, huku kukiwa na udhibiti wa uharibifu wa misitu kwa njia endelevu, bila kusahau kupambana na hali ya nchi kugeuka jangwa.

Linatia mkazo pia katika kukomesha uharibifu wa ardhi na kupiga vita vitendo vyote vinavyosababisha upotevu wa wanayama na mimea anuwai.

Serikali na wadau wote wanalojukumu la kuhamasisha jamii juu ya ushiriki wao katika kulinda, kusimamia maliasili za nchi hii kwa kuhakikisha unakuwepo ulinzi shirikishi wa kuwalinda wanyama wetu dhidi ya majangiri. 

Serikali imepiga hatua kubwa katika kulinda maliasili zote ikiwemo wanyamapori hapa nchini. Licha ya hatua kubwa hizo kumeendelea kuripotiwa vitendo vya ujangiri katika baadhi ya maeneo, huku watu mbalimbali wakiendelea kukamatwa wakiwa na nyara za serikali kama pembe za ndovu na meno ya tembo. Baadhi ya wanyamapori wameendelea kupoteza maisha kwa kugongwa na magari hasa nyakati za usiku kwenye hifadhi ambazo zimepitiwa na barabara.

Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda maliasili zetu kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na cha baadae.


Amani, Haki na Taasisi Madhubuti

Lengo hili limedhamiria kuendeleza jamii jumuishi na yenye amani kwa ajili ya maendeleo endelevu, huku ikitoa haki kwa wote na kujenga taasisi imara zenye kuwajibika katika nyanja zote. Linahimiza kudumisha usalama wa wananchi (raia) ambao unategemea sana uwepo wa taasisi zenye ufanisi, zenye kuwajibika, na zenye kuhusisha watu wote katika viwango vyote.

Serikali inalojukumu lakuhakikisha kunakuwa na utawala bora, utawala wa kufuata sheria, demokrasia, na haki inatolewa kwa wote bila upendeleo wowote ule. Inaowajibu pia wa wakuonesha ufanisi na uwajibikaji kwa wananchi wake kwa kuhakikisha inapambana na rushwa, na kuongeza uhuru wa wananchi kupata taarifa.

Licha ya kufanya vizuri katika kusimamia utawala bora na demokrasia nchini, bado kumekuwepo na malalamiko ya baadhi ya watumishi na watendaji wa serikali kutokufuata utawala wa sheria, ni wakati sasa wahusika wajitathimini na kufikiria upya namna nzuri ya kuweza kufanikisha lengo hili kwa kuhakikisha wanafuata utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.

Katika kupambana na rushwa serikali imefanya vizuri sana. Tumeshuhudia mafisadi wakifikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua stahiki. Licha ya kufanya vizuri katika kupambana na rushwa, vitendo vya rushwa vimeendelea kuripotiwa sehemu nyingi za nchi, hivyo naiomba serikali kuendeleza vita hii maana haki haiwezi kupatikana endapo kuna utitiri wa rushwa, na rushwa siku zote ni adui wa haki.

Baadhi ya kesi mahakamani zimeendelea kuchukua muda mrefu bila kusikilizwa huku watuhumiwa wakiendelea kusota rumande na mahabusu bila sababu za msingi. Watuhumiwa pia wameendelea kunyimwa dhamana hata kwa makosa ambayo yanastahili dhamana. Mabambiko ya kesi yameendelea kuwepo licha ya kupungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na siku za nyuma.

Matukio ya watu kutekwa, kupotea katika mazingira ya kutatanisha, na baadhi ya miili ya watu kuokotwa wakiwa wamekufa, ni miongoni mwa mambo yanayoenda kinyume na lengo hili. Ni wajibu wa seriklia na raia wote kuhakikisha wanakomesha jambo hili. Serikali ifuatilie matukio haya, na wananchi watoe ushirikiano kwa serikali kwa kutoa taarifa za matukio haya polisi kabla na baada ya kutokea.



Ushirikiano ili Kufanikisha Malengo

Kama ilivyo usemi usemao ‘umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu’, lengo hili linazitaka nchi zote na wadau wote kuendeleza ubia katika ngazi zote ili kuweza kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu. Linasisitiza juu ya kuimarisha njia za utekelezaji kwa kuunganisha nguvu na ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu.

Linahimiza juu ya ushirikiano katika masuala ya kifedha, teknolojia, biashara, masuala ya kisera, na masuala ya kuzijengea uwezo nchi maskini kuweza kutekeleza mipango yake. Linalenga kuimarisha uwezo wa nchi katika kusimamia na kukusanya mapato ya ndani, huku ikizitaka nchi zilizoendelea kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea (maskini) katika kufanikisha malengo yake.

Tumeona serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wa kimataifa na kitaifa katika kutekeleza malengo haya. Licha ya jitihada hizi kufanyika, mimi binafsi naona haitoshi hivyo naendelea kuomba ushirikiano zaidi toka pande nne za dunia katika kufanikisha malengo haya. Lazima tuhakikishe dunia inakuwa sehemu salama kwa binadamu kuishi huku akifurahia utu wake.

Serikali kuanzia ngazi ya serikali za mitaa hadi serikali kuu zinaowajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali, teknolojia pamoja na maarifa ya kutekeleza malengo yote endelevu. Hii ikiwa ni pamoja na serikali kuhakikisha inatenga fedha za kutosha kwa kila wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi maana tunaamini wizara zote zinatekeleza malengo haya.


HITIMISHO
Ni matumaini yangu kuwa baada ya kusoma makala hii fupi, kila mmoja wetu atafanya jitihada za kuhakikisha malengo haya 17 yanatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Malengo yote yanatekelezeka, tuungane kwa pamoja kuyatekeleza.

Thursday, June 28, 2018

TUTEKELEZE MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGs) [SEHEMU YA PILI]


Mara baada ya kuona lengo namba 1 hadi namba 5 katika makala iliyopita. Sasa tutazame lengo namba 6 hadi namba 10. Je unafahamu lengo namba 6 linahusu nini? vipi kuhusu lengo namba 7,8,9, na 10?, Utekelezaji wake ukoje? Basi karibu uungane nami katika mfululizo huu wa darasa kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).


Maji Salama na Usafi
Watu husema Maji ni Uhai, na Usafi ni Maisha.  Maji salama na usafi ni lengo la sita ambalo linaweka msisitizo katika upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na usafi kwa wote. Limelenga kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa watu wote ifikapo mwaka 2030. Hivyo linasisitiza jamii zote duniani kuhakikisha zinaongeza kasi katika kuongeza upatikanaji wa maji safi ya kunywa na kutumia kwa gharama nafuu, kupunguza uchafuzi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kemikali zenye sumu hazitiririki na kuathiri vyanzo vya maji, bila kusahau kuboresha maji taka kwaajili ya matumizi ya baadae.

Nchini Tanzania suala la upatikanaji maji salama na usafi limekuwa likifanyiwa kazi kwa kiwango chake, licha ya kutoonesha matokeo chanya mpaka sasa. Huduma ya upatikanaji maji safi na salama imekuwa ikiboreshwa kwenye maeneo mengi ya nchi lakini bado kumekuwa na kero ya ukosefu wa maji safi na salama. Kampeni ya kumtua mwanamke au mtoto wa kike ndoo, ilianzishwa kwenye maeneo mengi hapa nchini ikilenga kuhakikisha maji yanapatikana kwa karibu zaidi ili kumpunguzia kero mtoto wa kike kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.

Kwenya baadhi ya mikoa kama Dar es Salaam wameweka mfumo wa kuwawezesha wananchi kuunganishiwa maji kwa mkopo ili kuhakikisha wananchi wake wanaendelea kupata huduma ya maji huku wakifanya malipo polepole, jambo ambalo limesaidia wananchi wengi wasiokuwa na uwezo nao kupata fursa ya kunufaika na huduma ya maji. Kwa hili, mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kuwa mkoa wa mfano katika kutekelza Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kuhusu suala la usafi, kumekuwa na kampeni za kuhamasisha usafi katika maeneo yote ya nchi, kampeni ambazo ziliasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika miezi ya awali kabisa ya uongozi wake.  Katika kuunga mkono kampeni hii, mkoa wa Dar es Salaam uliandaa kampeni maalumu ya kusafisha jiji hilo ambalo awali lilikuwa likiongoza kwa uchafu hapa nchini, kampeni hiyo imeonesha mafanikio kwa kiasi chake ambapo kwasasa maeneo mengi ya jiji hilo la kibiashara ni masafi tofauti na hapo awali.

Licha ya mafanikio hayo kiduchu katika utekelezaji wa lengo hili, kero za ukosefu wa maji zimeendelea kuripotiwa kutoka kila kona ya nchi. Huku hali ikisemekana kuwa mbaya zaidi katika mikoa ya Kigoma, Singida, na Shinyanga. Hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika kuhakikisha maji salama yanapatikana kwa wananchi wote wa Tanzania.


Nishati Mbadala kwa Gharama Nafuu
Lengo hili limelenga kuhakikisha nishati mbadala kwa gharama nafuu inapatikana ili kumwezesha kila mmoja kumudu gharama zake. Nishati hiyo pia inategemewa kuwa endelevu na ya kisasa kwa watu wote. Serikali na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kuhakikisha zinapunguza matumizi ya nishati inayotokana na misitu.

Matumizi ya umeme wa uhakika unaotokana na nishati mbadala kama jua, upepo, na gesi yanasisitizwa. Hii itasaidia pia kuepusha hatari ya kutokea kwa jangwa kutokan na ukataji miti hovyo kwaajili ya kupata kuni za kupikia na kuchoma mkaa.

Nchini Tanzania jitihada mbalimbali zimefanywa na zinaendelea kufanywa katika kuhakikisha lengo hili linafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Wizara ya Nishati imeendelea kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi kupitia miradi yake mbali mbali, ukiwemo mradi wa REA ambao umekuwa ukisambaza umeme vijijini kwa gharama nafuu zaidi.

Licha ya upatikanaji wa nishati ya gesi hapa nchini, nishati hii haijaweza kuwasaidia wananchi kwani matumizi yake ni ya kiwango cha chini, pia upatikanaji wake umeendelea kuwa ghari licha ya nishati hiyo kupatikana hapa nchini. Inasikitisha zaidi kuona hata maeneo ya Mtwara ambako gesi inazalishwa wameendelea kutumia kuni huku gesi hiyo ikitumiwa  na wakazi wa miji mingine hapa nchini.

Licha ya serikali pia kujitahidi kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia watanzania wengi zaidi, maeneo mengi ya nchi yameendelea kubaki gizani bila huduma hiyo, huku baadhi ya maeneo ambayo tayari yana huduma hiyo yakiendelea kupata umeme husiokuwa na uhakika kufuatia katika katika umeme ya mara kwa mara ambayo imekuwa ikiyakumba maeneo hayo.

Ni wakati sasa wa serikali kuhakikisha inaongeza nguvu katika wizara ya nishati kwa kuitengea bajeti ya kutosha itakayoiwezesha kusimamia zoezi la usambazaji umeme katika maeneo mengi zaidi ya nchi. Ikimbukwe kuwa upatikanaji nishati mbadala ni suala lenye matokeo mtambuka kwani licha ya kutumika majumbani, umeme hutumika pia viwandani katika kuzalisha bidhaa mbalimbali na hivyo kuongeza pato la taifa.


Kazi zenye Staha na Ukuzaji Uchumi
Lengo hili linahimiza ukuaji endelevu wa kiuchumi wenye kujumuisha watu wote, huku kukiwa na uzalishaji wa ajira na kazi za staha kwa wote. Linahamasisha pia sera za maendeleo zinazosaidia shughuli za uzalishaji, ujasiriamali, ubunifu na uvumbuzi, huku likihimiza urasimishaji na ukuzaji makampuni na taasisi ndogo ndogo na za kati, ikiwa pamoja na kuhakikisha zinapatiwa huduma za kifedha.

Limedhamiria ifikapo mwaka 2030 kuwepo na ajira kamili na za uhakika kwa wanawake na wanaume wote, bila kusahau vijana na watu wenye ulemavu ikiwa sanjari na ujira sawa kwa kazi zenye thamani sawa. Linasisitiza pia suala la kupunguza kiasi cha vijana wasio na ajira, elimu au mafunzo ifikapo mwaka 2020.

Linahimiza pia nchi zote duniani kuchukua hatua za haraka na za ufanisi kuondoa kazi za kulazimisha, kukomesha utumwa wa kisasa na biashara ya binadamu. Suala la kukomesha aina zote za utumikiswaji watoto na matumizi ya wanajeshi watoto ifikapo mwaka 2025, limezungumziwa pia.
Lengo hili pia linazitaka nchi zote duniani kuhakikisha zinalinda haki za wafanyakazi na kuweka mazingira salama ya kazi kwa wafanyakazi wote, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wahamiaji, hasa wahamiaji wanawake, na wale walio katika kazi ngumu na hatarishi.

Nchini Tanzania utekelezaji wa lengo hili bado unasua sua. Tatizo la ajira kwa vijana limeongezeka mara dufu, huku vyuo vikiendelea kuzalisha wasomi na watalaamu ambao baada ya kuhitimu masomo yao wanasota mtaani bila kupata ajira toka serikalini. Utumikiswaji wa watoto katika shughuli mbalimbali ikiwemo kazi za nyumbani (ndani) umeendelea kuwepo licha ya hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na serikali kukomesha utumikiswaji wa watoto.

Haki za wafanyakazi bado hazifuatwi. Wafanyakazi wawekuwa wakisimamishwa na kufukuzwa kazi bila kufuatwa kwa utaratibu. Wengine wamekuwa wakikosa stahiki zao wanazostahili mara baada ya kuwa wamefutwa au kusimamishwa kazi. Ni wakati sasa kwa serikali ya Tanzania kutazama suala la haki za wafanyakazi hapa nchini, ikiwa pamoja na kuwaandalia mazingira mazuri ya kufanyia kazi.


Viwanda, Ubunifu na Miundombinu
Lengo hili linalenga kuhimiza nchi zote duniani kujenga miundombinu imara, kukuza viwanda jumuishi na endelevu, na kuchochea ubunifu (uvumbuzi). Limedhamiria kukuza miundombinu yenye ubora na kuaminika inayozingatia jiografia ya maeneo husika hasa vijijini ili kusaidia ustawi wa maendeleo ya kiuchumi kwa wote.

Linalenga pia kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, ikiwa pamoja na mikopo yenye masharti nafuu kwa viwanda vidogo vidogo, na kwa wazalishaji wengine. Jambo hili sharti liende sambamba na kuhakikisha masoko yanapatikana kwa ajili ya bidhaa zinazozalisha na viwanda hivi vidogo vidogo.

Lengo hili pia linazitaka nchi zote mwanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la upatikanaji wa habari na teknolojia ya mawasiliano, pamoja na huduma nafuu ya mtandao (internet) kwa nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2020.

Suala la uanzishwaji wa viwanda nchini Tanzania limefanikiwa kwa kiasi chake chini ya uongozi wa awamu ya tano ambao umeweka mkazo katika uchumi wa viwanda. Viwanda mbalimbali vimeanzishwa katika maeneo tofauti ya nchi ikiwemo mkoani Simiyu ambako wameanzisha kiwanda cha chaki kinachohudumia mkoa huo pamoja na maeneo mengine ya jirani.

Licha ya mafanikio hayo katika uanzishwaji viwanda nchini, dhana ya viwanda kwa wananchi wa Tanzania bado haijaeleweka vizuri, huku wananchi wakitaka ufafanuzi zaidi kuhusu dhana ya ‘kiwanda kwa vyerehani vinne’ kama ilivyoelezwa na mamlaka yenye kusimamia sekta ya viwanda nchini.


Kupunguza Tofauti
Lengo hili linalenga kupunguza hali ya kutokuwepo kwa usawa ndani na miongoni mwa nchi mbalimbali hapa duniani. Linasisitiza juu ya uwezeshaji na ushirikishwaji jumuishi wa shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa watu wote bila kujali umri, jinsia, ulemavu, ukabila, asili ya mtu, dini, hali ya kiuchumi, au hali yoyote ile.

Linalenga pia kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa fursa na kupunguza tofauti ya kimatokeo, ikiwa ni pamoja na kuondoa sheria, sera na taratibu za kibaguzi, na kuhamasisha sera na hatua zenye kuhimiza usawa kwa wote. Linasisitiza juu ya kuimarisha sheria na taratibu juu ya usimamizi wa masoko ya kifedha zitakazokuwa na sura ya usawa kwa mataifa yote.

Linadhamiria pia kuhakikisha kunakuwepo na uwakilishwaji sawa katika kufikia maamuzi ya masuala mbalimbali ya kimataifa ikiwemo uchumi na fedha ili kujenga mazingira ya uwazi na uwajibikaji kwa mataifa yote. Vilevile linasisitiza juu ya kutekelezwa kwa sera zenye kutoa upendeleo maalumu wa huduma kwa nchi zinazoendelea kwa kuzingatia makubaliano na shirika la biashara duniani.

Nchini Tanzania bado kumeendelea kuwepo na tofauti kubwa ya kimaendeleo kati ya maeneo ya mjini na vijijini, hali inayoonesha kutofanikiwa kwa lengo hili hapa nchini. Huduma za kijamii na kiuchumi kama barabara zimebaki kuwa changamoto kubwa katika maeneo mengi ya vijijini ukilinganisha na maeneo ya mjini.

Wakati wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakifurahia usafiri safi na wa haraka wa mwendo kasi, hali ni tofauti kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma ambao hawategemei kabisa kupata huduma hiyo katika kipindi hiki. Huduma za kifedha kama benki bado hazijafika kwenye baadhi ya maeneo ya vijijini na hivyo kuwalazimu wakazi wa maeneo husika kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za kifedha.

Mara baada ya kuangalia lengo namba 6 hadi namba 10, Je kwa upande wako una nini cha kuongezea kuhusu malengo haya? Je, ni kweli hakuna mtu aliyeachwa nyuma katika utekelezaji wa malengo haya?, Je wewe binafsi upi ni mchango wako katika kuhakikisha kuwa hadi ifikapo mwaka 2030 malengo haya yanakuwa yametekelezwa kikamilifu?

FAHAMU KUHUSU MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGs)


SHULE INAYOTOA MICHEZO KAMA HII INAFAA KWA MZAZI NA MLEZI KUPELEKA MTOTO WAKE