SURA YA NANE
KULEA MTOTO
Nani anaweza kuwa mlezi?
(i) Mtu yeyote mwenye umri juu ya
miaka ishirini na moja, mwenye maadili mema na tabia njema, anaweza kuwa mlezi
wa mtoto.
(ii) Mlezi, kama ilivyotumika
katika sehemu hii, ni mtu ambae siyo mzazi wa mtoto lakini ana hiari na uwezo wa
kumtunza na kumkimu mtoto.
(iii) Kamishna anaweza kumweka mtoto
chini ya mlezi pale:
(a) Mtoto anapopelekwa katika makazi yaliyoidhinishwa
au taasisi chini ya amri ya
usimamizi;
(b) Mapendekezo yanapofanywa na Ofisa
wa Ustawi wa Jamii kwamba makazi
yaliyoidhinishwa au taasisi ni mahali
panapomfaa mtoto; au
(c) Mtoto anapokuwa amewekwa na mtu
yeyote katika makazi yaliyoidhinishwa au taasisi.
(iv) Maombi ya kumlea mtoto
yatafanywa kwa Kamishna, ambaye atayapeleka kwa Ofisa waUstawi wa Jamii, mlezi
au mtu aliye na mamlaka katika makazi yaliyoidhinishwa.
(v) Mlezi ambaye mtoto amewekwa chini
ya matunzo na malezi yake atakuwa na majukumu ya kumlea na kumkimu mtoto sawa
na majukumu aliyonayo mzazi wa mtoto.
(vi) Mtoto aliyewekwa chini ya malezi
atakuwa na haki ya kuabudu kulingana na imani ya dini yake wakati alipozaliwa.
(vii) Mlezi anayekiuka sheria kama
ilivyoainishwa sehemu hii atakuwa ametenda kosa chini ya sheria hii.
SURA YA TISA52
KUASILI MTOTO
Kutoa Amri ya Kuasili
Maombi ya kuasili yanafanywa wapi?
(i) Kwa kuzingatia sheria kama
ilivyoainishwa katika
Sheria hii:
(a) Maombi ya kuasili mtoto yanaweza
kufanywa Mahakama Kuu;
(b) Maombi kwa ajili ya “kuasili
kwa wazi” yatafanywa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi au Mahakama ya Wilaya.
(ii) Baada ya kupokea maombi,
Mahakama inaweza kutoa amri ya kuruhusu maombi ya kuasili au kuasili kwa wazi
kulingana na Sheria hii.
(iii) Maana ya kuasili kwa wazi”
kama ilivyotumika katika sheria hii, ni kuasili mtoto kunakofanywa na ndugu.
53
Ni nani anaweza kuomba kuasili?
Maombi ya kuasili
(i) Maombi ya amri ya kuasili
yanaweza kufanywa kwa pamoja na
(a) Mume na mke; au
(b) Mama au baba wa mtoto peke yake
au pamoja na mwenzi wake.
(ii) Kuhusu maombi ya kuasili kwa
wazi, maombi hayo yanaweza kufanywa na ndugu wa mtoto.
54
Ridhaa ya Wazazi na Walezi
(i) Amri ya kuasili itatolewa tu
kunapokuwa na ridhaa ya wazazi au walezi wa mtoto.
(ii) Mahakama inaweza kutohitaji
ridhaa ya wazazi, walezi au ndugu wa mtoto kama itaridhika kwamba:
(a) Wazazi, walezi au ndugu
wamemtelekeza mtoto au wamekuwa wakimtendea mtoto vibaya kwa muda mrefu.
(b) Au kama mtu hawezi kupatikana au
hana uwezo wa kutoa ridhaa.
(c) Au kama hakuna sababu ya maana ya
kutokutoa ridhaa.
(iii) Mzazi yeyote, mlezi au ndugu wa
mtoto ambaye anahusika katika maombi ya kuasili au ametoa ridhaa kwa ajili ya
amri ya kuasili hatastahili kumtoa mtoto kutoka kwa mwombaji. Itakuwa hivyo tu
kama ana kibali cha mahakama na itakuwa kwa manufaa ya mtoto.
Amri ya kuasili
Je, mtoto aliyeasiliwa ana haki ya
kupewa taarifa ya uasili?
(i) Mzazi aliyeasili atamfahamisha
mtoto aliyeasiliwa kwamba ameasiliwa. Atamfahamisha pia kuhusu nasaba yake.
Lakini, taarifa hii itatolewa kama:
(a) Ni kwa ajili ya manufaa ya mtoto;
na
(b) Mtoto ana umri angalau wa miaka
kumi na nane.
(ii) Mtu mwingine hana ruhusa ya
kutoa taarifa kwamba mtoto ameasiliwa isipokuwa mzazi wa kuasili.
(iii) Mtu yeyote anayekiuka kifungu
hiki anatenda kosa. Akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini ya si chini ya
shilingi mia moja elfu, lakini isiyozidi shilingi milioni mbili au kifungo cha
muda usiozidi miezi kumi na mbili au vyote kwa pamoja.
Maombi yaliyofanywa na Mtu Asiyekuwa
Mkazi
(i) Katika maombi ya kuasili
yaliyofanywa na mwombaji ambaye ni raia wa Tanzania, lakini haishi ndani ya Tanzania,
mahakama itajiridhisha kwamba kuna taarifa za kutosha kuweza kufanya maombi,
kisha itatoa amri ya muda.
Vilevile, kama maombi ya pamoja
yamefanywa, na mmoja wa waombaji si mkazi wa Tanzania, mahakama itajiridhisha kwamba
kuna taarifa za kutosha kuweza kufanya maombi, kisha itatoa amri ya muda.
(ii) Mahakama itajiridhisha kwamba
kuna taarifa za kutosha kutoka kwa mamlaka inayotambulika kule mwombaji
anakoishi na kwenye nchi yake ya asili, ndipo itoe amri ya muda au amri ya
kuasili.
Watoto ambao waliasiliwa kabla
(i) Amri ya kuasili au amri ya muda
inaweza kufanywa kwa ajili ya mtoto ambaye ameshaasiliwa na wazazi wa kuasili .
Kama wazazi wa kuasili wa awali bado wako hai, watachukuliwa kuwa ni wazazi au
walezi wa mtoto kwa lengo la kuasili kunakofuata.
Athari za Kuasili kwa haki za Mzazi
(i) Wakati amri ya kutoa amri ya
kuasili:
(a) Haki, wajibu na majukumu
yanayotokana na kuasili yana ukomo. Haya ni pamoja na yale yanayotokana na
sheria za mila na desturi za wazazi wa mtoto, au mtu yeyote anayehusiana na
mtoto.
(b) Haki, wajibu na majukumu ya
wazazi vitakuwa chini ya mzazi wa kuasili ambaye anachukua nafasi ya mzazi wa
mtoto. Hii inajumuisha majukumu yote kuhusu uangalizi, kukimu na elimu ya
mtoto, kama vile mtoto alizaliwa na wazazi wa kuasili kisheria katika ndoa yao,
na hakuwa mtoto wa mtu mwingine .
(ii) Pale ambapo amri ya kuasili
imetolewa kwa mume na mke kwa pamoja, wote kwa pamoja watachukua majukumu ya wazazi
kama vile wamemzaa mtoto wao wenyewe kiasili kama mume na mke.
Kuasili na Sheria za Kimila
(i) Mtoto wa kuasili atakuwa chini ya
sheria za kimila kama vile alikuwa mtoto wa kuzaliwa wa wazazi wa kuasili kama
wazazi wa kuasili wako chini ya sheria za kimila.
Usajili wa Watoto Walioasiliwa
(i) Amri ya kuasili iliyotolewa na
mahakama itakuwa na maelekezo kwa Msajili Mkuu kuweka kumbukumbu katika Rejesta
ya Watoto Walioasiliwa.
(ii) Kwa ajili ya kutimiza mahitaji
ya kumbukumbu ya rejesta, ambapo:
(a) Tarehe halisi ya kuzaliwa mtoto
haijathibitika kuweza kuiridhisha mahakama, mahakama itaamua tarehe inayoelekea
kuwa tarehe ya kuzaliwa kwa mtoto. Tarehe hiyo itatajwa kwenye amri.
(b) Jina au ubini litakalotumika kwa
mtoto likiwa tofauti na lile la awali, jina jipya litatajwa kwenye amri badala
ya jina la zamani.
(c) Nchi aliyozaliwa mtoto
haijathibitika kuweza kuiridhisha mahakama, taarifa za nchi hiyo zinaweza kuachwa
katika amri ya kuasili. Nchi haitawekwa pia kwenye Rejesta ya Watoto Walioasiliwa.
(iii) Kwa mtoto ambaye alikuwa
hajaasiliwa, maelezo ya kwamba “Ameasiliwa” yatatolewa kwa Msajili Mkuu na
kuwekwa kwenye taarifa za Rejesta ya Vizazi. Hili litafanyika baada ya mahakama
kupokea maombi ya amri ya kuasili na kujiridhisha kwamba taarifa zinaendana na
zile zilizo kwenye Rejesta ya Vizazi.
(iv) Pale ambapo amri ya kuasili
imetolewa na mahakama chini ya sheria hii, mahakama itawasilisha maelekezo kwa
Msajili Mkuu. Baada ya kupokea mawasiliano hayo,Msajili Mkuu atawezesha
maelekezo yaliyoko kwenye amri ya mahakama yatekelezwe yote. Neno “Ameasiliwa”
litawekwa kwenye Rejesta ya Vizazi na katika Rejesta ya Watoto Walioasiliwa.
Kuasiliwa na Mtu Asiye Raia
Je, mtoto anaweza kuasiliwa na mtu
ambaye sio Mtanzania?
(i) Mtu yeyote ambaye siyo raia wa
Tanzania anaweza kuasili mtoto ambaye ni Mtanzania. Hilo linawezekana kama:
(a) Mtoto hawezi kuwekwa chini ya
malezi au kwenye familia ya kuasili. Au kama mtoto hawezi kutunzwa katika hali
ambayo inafaa kwa ajili ya ustawi wake akiwa Tanzania.
(b) Mtu anayetaka kuasili ameishi
Tanzania kwa muda wa miaka mitatu mfululizo;
(c) Amemlea mtoto kwa muda wa miezi
mitatu chini ya usimamizi wa Ofisa Ustawi wa Jamii;
(d) Hana historia ya kutenda makosa
ya kijinai katika nchi aliyotoka au nchi nyingine yoyote;
(e) Amependekezwa kuwa anafaa
kumuasili mtoto kutoka kwa Ofisa wa Ustawi wa Jamii. Au kama amependekezwa na
mamlaka yenye uwezo katika nchi ambako anaishi.
(f) Ameiridhisha mahakama kwamba nchi
alikotoka inaheshimu na inatambua amri ya
kuasili.
(ii) Kwa kuzingatia kifungu kidogo
cha (i) , mahakama inaweza kutoa amri ya kuasili
kama ni kwa ajili ya manufaa ya
mtoto.
(iii) Kwa ajili ya maombi ya kuasili
ya mtu ambaye sio raia wa Tanzania, Ofisa Ustawi wa Jamii atatakiwa kufanya
uchunguzi. Ofisa wa Ustawi wa Jamii atatoa ripoti ya uchunguzi wa kijamii ili
kuisaidia mahakama kufanya uamuzi kuhusu maombi.
(iv) Mahakama inaweza kutoa amri ya
ziada kuhusiana na maombi ya kuasili ya mtu
asiye raia wa Tanzania:
(a) Kumtaka Ofisa wa Ustawi wa Jamii kuwakilisha
maslahi ya ustawi wa mtoto;
(b) Kumtaka Ofisa wa Ustawi wa Jamii
kuandaa ripoti ya uchunguzi wa kijamii ili kuisaidia mahakama kufanya maamuzi,
iwapo amri ya kuasili itakuwa kwa manufaa ya mtoto au la;
(c) Suala lolote ambalo mahakama inaweza
kuamua.
No comments:
Post a Comment