SURA YA KUMI
KURITHI MALI
Kugawa Mali bila Wasia
Je, mtoto aliyeasiliwa atarithi mali
zipi?
(i) Pale mzazi wa kuasili anapofariki
bila kuacha wasia, mali zake zinakuwa mali za mtoto wa kuasili, kama vile mtoto
amezaliwa na wazazi wa kuasili.
(ii) Kwa ajili ya kuondoa utata,
mtoto wa kuasili hatastahili kurithi mali kama wazazi wake wa kibaiolojia
wakifa bila kuacha wasia.
Kugawa Mali kwa Wasia
(i) Mgawanyo unaofanywa baada ya
tarehe ya amri ya kuasili, iwe mali halisi au binafsi, iwe au isiwe kwa maandishi,
itazingatia:
(a) Maelezo yoyote yenye marejeo, yaliyo
wazi au kwa kuhisi, yanayohusu mtoto wa mzazi wa kuasili, yanamhusu pia mtoto
wa kuasili, isipokuwa kama itaonyeshwa vinginevyo.
(b) Pale ambapo mgao ulifanywa na
mzazi wa kuasili kabla ya tarehe ya kutolewa amri ya kuasili, na mtoto wa kuasili
hakutajwa katika mgao huo, mtoto wa kuasili anaweza kuomba mahakamani ili mgao
huo uweze kubadilishwa, ili naye ahusishwe katika mgao.
(c) Marejeo yoyote kwa wazazi wa
mtoto wa kuasili katika wasia, hayatatafsiriwa kumhusisha mtoto aliyeasiliwa,
isipokuwa kama kutakuwa na nia ya kufanya hivyo.
(d) Marejeo yoyote kwa ndugu wa mzazi
wa kuasili, hayatatafsiriwa kuwa yanarejea kwa mtu huyo kama vile ni ndugu wa
mtoto aliyeasiliwa, isipokuwa kama kutakuwa na nia ya kufanya hivyo.
(ii) Mgao katika wasia unaofanywa
kabla ya tarehe ya amri ya kuasili hautachukuliwa kama vile umefanywa baada ya
tarehe ya amri ya kuasili. Kiambatisho cha wasia cha tarehe kabla ya amri ya
kuasili hakiwezi kukubalika.
(iii) Mgao, lina maana ya
kuhamisha masilahi katika mali kwa hati yoyote, iwe kwa watu walio hai, au kwa wasia,
ikiwa ni pamoja na kiambatisho cha wasia.
63
SURA YA KUMI NA MOJA
AJIRA YA MTOTO
Haki ya Mtoto Kufanya Kazi
(i) Mtoto atakuwa na haki ya kufanya
kazi nyepesi.
(ii) Pamoja na kwamba mtoto ana haki
ya kufanya kazi nyepesi, umri wa chini wa kuajiri mtoto utakuwa miaka kumi na
nne.
Kazi nyepesi ni zipi?
(iii) Kazi nyepesi”
itahusisha kazi ambayo haiwezi kuwa na madhara kwa afya ya mtoto, au kwa maendeleo
yake. Kazi hiyo haitamzuia au haitaathiri mahudhurio ya mtoto ya shule,
kushiriki katika shughuli za kujiendeleza kiufundi au programu ya mafunzo au
uwezo wa mtoto kunufaika na kazi za shule.
Kukataza Kazi za Kiunyonyaji
(i) Mtu hataruhusiwa kumuajiri au
kumshughulisha mtoto katika aina yoyote ya kazi itakayomnyonya mtoto.
(ii) Bila kupingana na kifungu hiki
cha sheria, kila mwajiri atahakikisha kuwa kila mtoto aliyeajiriwa kihalali na
kulingana na sheria hii, analindwa.
Mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya
kutengwa au matendo yoyote yanayoweza kuwa na athari mbaya kwake kwa kuzingatia
umri na uwezo wake.
(iii) Nini maana ya kazi za
kinyonyaji?
Kazi itakuwa ni ya kinyonyaji iwapo:
(a) Inamnyima mtoto kuwa na afya
njema au maendeleo;
(b) Ni ya muda zaidi ya saa sita kwa
siku;
(c) Haifai kwa umri wake; au
(d) Mtoto hapati malipo ya kutosha
(iv) Mtu yeyote anayevunja sheria
katika kifungu hiki anatenda kosa. Akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini
isiyopungua shilingi laki moja au kutumikia kifungo kwa muda wa miezi mitatu au
vyote kwa pamoja.
Ni katika kazi zipi mtoto hawezi
kuajiriwa?
Kukataza Kazi za Usiku
(i) Bila kupingana na sheria hii,
mtoto hataajiriwa au kuhusishwa katika mkataba wa huduma ambayo itamuhitaji
mtoto afanye kazi usiku.
(ii) “Kazi ya usiku” ni kazi
inayohusu utendaji unaohitaji mtoto awe kazini kati ya saa mbili jioni na saa
kumi na mbili asubuhi.
(iii) Mtu yeyote anayevunja sheria
katika kifungu hiki anatenda kosa. Akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini
isiyopungua shilingi laki moja au kutumikia kifungo kwa muda wa miezi mitatu au
vyote kwa pamoja.
66
Kukataza Ajira ya Lazima
(i) Mtu yeyote atakayemshawishi,
atakayempeleka, atakayemtaka au atakayemlazimisha mtoto kufanya kazi kwa lazima
anatenda kosa.
(ii) Kwa madhumuni ya kifungu hiki, ‘ajira
ya muda” inahusisha kazi ya kitumwa au kazi yoyote inayofanyika
kwa vitisho vya adhabu. Ajira ya muda haihusishi kazi za kawaida
za kijamii, kazi ndogondogo za huduma kwa jamii zinazofanywa
na wanajumuiya kwa manufaa ya jamii.
(iii) Mtu yeyote anayevunja sheria
katika kifungu hiki anatenda kosa. Akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini
isiyopungua shilingi laki mbili au kutumikia kifungo cha muda wa miezi sita au
vyote kwa pamoja.
Haki ya Kulipwa Ujira
(i) Mtoto ana haki ya kulipwa ujira
sawa na thamani ya kazi aliyofanya.
(ii) Licha ya sheria kama
ilivyoainishwa katika Sheria ya Kazi na Uhusiano wa Kikazi, mwajiri yeyote ambaye
anakiuka sheria katika kifungu hiki anatenda kosa.
67
Ajira ya Hatari
(i) Siyo halali kisheria kumuajiri au
kumhusisha mtoto kwenye kazi ya hatari.
Ajira za hatari ni zipi?
(ii) Kazi ya hatari ni
kazi yoyote inayoweza kuleta hatari kwa afya, usalama na maadili ya mtoto.
(iii) Kazi ya hatari itahusisha:-
(a) Kwenda baharini;
(b) Kufanya kazi migodini au kuchimba
na kupasua kokoto;
(c) Kubeba mizigo mizito;
(d) Kufanya kazi katika viwanda vya
uzalishaji ambako kemikali zinatengenezwa au kutumika;
(e) Kufanya kazi sehemu ambako
mashine zinatumika; na
(f) Kufanya kazi sehemu za baa,
hoteli au sehemu nyingine za starehe.
(iv) Pamoja na kwamba kazi za hatari
zimeainishwa na kuzuiwa, sheria yoyote iliyoandikwa inayosimamia mafunzo
inaweza kumruhusu mtoto:
(a) Kuingia katika merikebu ili
ahudhurie mafunzo kama sehemu ya mafunzo ya mtoto;
(b) Katika kiwanda au mgodi, kama
kazi ni sehemu ya mafunzo ya mtoto;
(c ) Katika sehemu yoyote ya kazi kwa
masharti kwamba afya, usalama, na maadili ya mtoto vitalindwa na mtoto amepata
au anapata maelekezo maalumu, au mafunzo yanayoendana na kazi au shughuli hiyo.
Kumtumia Mtoto kwa Shughuli za
Kikahaba
(i) Mtoto hataajiriwa katika kazi
yoyote au biashara inayomweka mtoto katika mazingira ya ngono, iwe kwa malipo
au la;
(ii) Kwa kuondoa utata, itakuwa ni
kukiuka sheria kwa mtu yoyote kutumia:
(a) Ushawishi au kumlazimisha mtoto
ashiriki katika vitendo vya ngono;
(b) Watoto katika vitendo au shughuli
zozote za umalaya;
(c) Watoto katika kutengeneza picha
au maandishi yenye kutia ashiki.
(iii) Mtu yeyote anayevunja sheria
katika kifungu hiki anatenda kosa. Akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini
isiyopungua shilingi milioni moja na isiyozidi shilingi milioni tano au
kutumikia kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na usiozidi miaka
ishirini au vyote kwa pamoja.
Sheria juu ya kazi za hatari
itatumika sehemu gani?
(i) Kwa kuzuia utata, sehemu hii
itatumika kwa ajira katika sekta rasmi na isiyo rasmi.
(ii) Kwa kuzingatia kifungu kidogo
cha (i), Ofisa wa Kazi, katika muda muafaka, ataingia katika nyumba au sehemu
ya nyumba na kufanya ukaguzi kama ataona ni lazima, ili kujiridhisha kwamba
sheria katika sehemu hii inatekelezwa.
(iii) Neno “nyumba” lina
maana ya nyumba, shirika, kampuni, ofisi, uwanja, shamba, eneo; na inahusisha
chombo, merikebu, gari na ndege.
70
Usajili wa Mtoto katika Sehemu za
Kazi
Je, taarifa zinazohusu mtoto katika
sehemu ya kazi ni zipi?
(i) Mwajiri, katika sehemu za kazi,
atatunza rejesta ya watoto walioajiriwa naye, tarehe za kuzaliwa kwao, kama zinafahamika
au umri unaodhaniwa kuwa ndio umri wao, kama tarehe zao za kuzaliwa hazijulikani.
(ii) Shughuli za kikazi ni shughuli
nyingine ambazo si za kibiashara au kilimo. Shughuli za kikazi zinajumuisha:
(a) Migodi, machimbo ya mawe, na kazi
nyingine za kuchimba madini kutoka ardhini.
(b) Shughuli ambazo kutokana nazo,
vitu mbalimbali vinatengenezwa, vinabadilishwa,
vinasafishwa, vinakarabatiwa,
vinapambwa, vinaboreshwa, vinatwaliwa kwa kuuzwa,
vinavunjwa au kuharibiwa, au ambako
vitu vinabadilishwa. Zinajumuisha shughuli za
kujenga merikebu au shughuli za
kufua, kubadili na kusambaza umeme au nishati ya
aina yoyote.
(c) Shughuli za kusafirisha abiria au
bidhaa kwa barabara au reli pamoja na kushughulikia bidhaa katika gati,
kikwezo, ghala na uwanja wa ndege.
71
Utekelezaji wa Sheria
Sheria ya ajira kwa watoto
inafuatiliwa na nani? Wakati gani?
(i) Ofisa wa Kazi atafanya uchunguzi
wowote kama anaona ni lazima ili kujiridhisha kwamba sheria katika sehemu hii
kuhusu ajira ya watoto zinatekelezwa kwa hakika.
(ii) Ofisa wa Kazi anaweza kumusaili
mtu yeyote kama ni lazima.
(iii) Pale ambapo Ofisa wa Kazi kwa
busara zake ameridhika kwamba sheria katika kifungu hiki haitekelezwi, atatoa
amri ya kutokutekelezwa kwa sheria katika ajira. Ofisa wa Kazi atapeleka ripoti
kwa Ofisa Ustawi wa Jamii na kituo cha polisi kilicho karibu. Ofisa wa Ustawi
wa Jamii na polisi watafanya upelelezi na kuchukua hatua zinazofaa ili kumlinda mtoto.
No comments:
Post a Comment