Kumekuwepo na
changamoto ya ajira kwa vijana wengi wanaohitimu masomo yao katika nchi nyingi
za Afrika. Nchini Tanzania kuna vijana waliohitimu masomo yao kwa takribani
miaka mitatu (3) sasa (2015 – 2018), ambao bado hawana ajira na hakuna mpango
wowote wa matumaini kwa vijana hawa kupata au kupewa ajira na wenye mamlaka.
Kumekuwepo na
kurushiana mpira kwa nani haswa anapaswa kulaumiwa katika changamoto hii ya
ajira kwa vijana hasa wale waliohitimu masomo yao katika vyuo mbalimbali hapa
nchini, ikizingatiwa kuwa wengi wa vijana hawa walisoma masomo ambayo
yanahitaji kuajiriwa, hii ni kulingana na mazingira halisi ya nchi nyingi za
Afrika.
Mtizamo wa Viongozi na
wenye Mamlaka ya Kutoa Ajira ukoje?
Viongozi wengi na wenye
mamlaka ya kutoa ajira wamekuwa wakirusha lawama zao kwa vijana na kuwatuhumu
kuwa wamekuwa ni vijana wazembe wasioweza kujiajiri na akili zao zinawaza
kuajiriwa tu. Jambo hili limekuwa likipingwa na vijana wengi hasa wahitimu wa
vyuo vikuu ambao wamekuwa na mtizamo tofauti na viongozi wao.
Mtizamo wa vijana juu
ya ukosefu wa ajira ukoje?
Vijana wengi ambao ndio
wahanga wakubwa wa tatizo la ajira wamekuwa wakilalamikia mazingira magumu
ambayo kwao ndio tatizo kubwa linalopelekea kushindwa kuajiriwa na kujiajiri.
Mazingira haya yanatajwa kusababishwa na mfumo mbovu ambao umekuwa ukikumbatiwa
na waajiri, viongozi, na wenye mamlaka ya kuajiri. Miongoni mwa sababu ambazo
zinatajwa na vijana wengi kuwa changamoto kwao katika kuajiriwa na kujiajiri ni
hizi zifuatazo:
Mfumo mbovu wa Elimu.
Vijana wengi wamekuwa
wakilalamikia mfumo mbovu wa elimu ambao badala ya kuwaandaa kujiajiri umekuwa
ukiwaandaa kuajiriwa. Sababu hii imekuwa ikitolewa na wengi wa vijana ambao
wamesoma masomo ya sanaa (Arts) hasa katika fani ya ualimu. Vijana hawa
wanasema kuwa toka mwanzo walipokuwa wanafanya udahili wa kujiunga katika masomo
yao walifahamu kuwa (na huo ndio ulikuwa utaratibu) punde tu watakapohitimu
masomo yao wataajiriwa na serikali, jambo ambalo limekuwa tofauti kabisa na
matarajio yao ambapo sasa wanaambiwa wajiajiri. Swali ambalo wanajiuliza vijana
hawa ni kwamba, “Je, tunajiajiri vipi? tunaanzisha
shule zetu za kufundisha masomo yetu ya sanaa au tunafanyaje?, kama ndivyo, je
tunapata wapi pesa za kugharamia miundombinu ya shule?, na je kama sisi hatuna
ajira na serikali haitaki kutuajiri tutapata wapi wanafunzi ambao watakuja
kwetu kujifunza angali wanafahamu kuwa wakihitimu masomo yao hawana mahali
pakwenda?. Hayo ni baadhi tu ya maswali ambayo vijana hawa wanajiuliza, mimi mwenyewe sijui majibu yake, msomaji
wangu kama unafahamu basi utatuambia nasisi tufahamu.
Ugumu wa Mazingira ya Kujiajiri.
Sababu nyingine inayotolewa
na vijana juu ya kwanini haswa hawajiajiri ni Mazingira Magumu ya Kujiajiri. Wamekluwa wakilalamika kukosa mitaji
itakayowawezesha kuanzisha biashara ndogo ndogo za kuweza kujipatia kipato.
Baadhi yao wamekuwa wakijaribu kuomba msaada kutoka kwa viongozi wa serikali (ambao
wamekuwa wakisisitiza vijana kujiajiri) lakini viongozi hao wamekuwa hawatoi
msaada wowote kwa vijana hao na badala yake wamekuwa wakitumia vyombo vya
habari kuwataka vijana wajiajiri. Mbaya zaidi katika hili ni baadhi ya viongozi
kutokuwajibu kabisa vijana hawa pale wanapowatumia barua pepe, barua ya
kawaida, meseji za simu, na hata kuwapigia simu, wakiomba kusaidiwa kwa
kuwaeleza mipango (projects) zao.
Kuna baadhi ya vijana
ambao familia zao kidogo zina uwezo hivyo wamebahatika kupewa mitaji ya biashara
na wanafamilia. Hawa nao wamekuwa wakilalamika kusumbuliwa na wenye mamlaka kwa
kutozwa kodi kubwa inayopelekea kufunga biashara zao kutokana na kutokuwa na
uhusiano kati ya kodi na mauzo yanayopatikana, kukosekana kwa maeneo ya
kufanyia biashara zao, na kukosekana kwa wateja kutokana na mzunguko wa fedha
kusuasua katika maeneo mengi ya nchi.
Ubinafsi na Kujuana katika fursa za
Ajira.
Hii ni sababu nyingine
ambayo vijana wengi wamesikika wakiitaja kama moja ya changamoto ya wao kupata
ajira. Kumekuwepo na masuala ya ubinafsi na kujuana katika kupata nafasi za
kazi katika nchi nyingi za Afrika. Nchini Tanzania vijana wanawalaumu viongozi
wa serikali kukumbatia kasumba hii. Inasemekana kuwa nafasi za kazi na ajira
zimekuwa zikitolewa kwa ubaguzi na kujuana, mathalani waziri kutoka eneo fulani
huwajaza vijana kutoka eneo lake kwenye vitengo mbalimbali vya wizara yake.
Suala la uchama nalo limekuwa likitajwa kama kikwazo, vijana wasio na vyama na
wale wa upinzani wamekuwa wakiwatuhumu viongozi wa serikali kuwapendelea vijana
walio upande wa chama tawala.
HIZO NI BAADHI TU YA
SABABU ZINATOTAJWA KAMA KIKWAZO KATIKA SUALA LA AJIRA KWA VIJANA. JE KUNA
SABABU ZINGINE UNAZIFAHAMU ZIMESAHAULIKA? BASI ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
KWENYE SEHEMU YA MAONI (COMMENTS). AHSANTE!
No comments:
Post a Comment