Mara baada ya kuona lengo namba 6 hadi namba 10
katika makala iliyopita. Sasa tutazame lengo namba 11 hadi namba 17. Je
unafahamu lengo namba 11 linahusu nini? vipi kuhusu lengo namba 12, 13,14, 15, 16, na 17?,
Utekelezaji wake ukoje? Basi karibu uungane nami katika sehemu ya tatu ya mfululizo huu wa darasa
kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Miji
na Jamii Endelevu
Lengo
hili linalenga kuweka miji, majiji, na makazi ya watu kuwa jumuishi, salama,
imara na endelevu. Linasisitiza serikali na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa
kuhakikisha zinazuia ujenzi holela kwa kuweka mipango miji na kuhakikisha
zinatenga maeneo maalumu kwaajili ya ujenzi wa maeneo ya kijamii kama viwanja
vya mipira, masoko, na nyumba za serikali.
Vile
vile linalenga kuzuia ujenzi wa makazi kwenye maeneo hatarishi, na kwa yale
ambayo tayari watu washajenga basi wapewe mahali salama kwa ajili ya makazi.
Linasisitiza pia ujenzi wa miundombinu ya usafiri kwa umma kuzingatia watu
wenye mahitaji maalumu kama walemavu, wazee na watoto.
Linahimiza
pia kuweka mipango mikakati ya kuendeleza huduma za msingi vijijini ili kuwepo
uwiano kati ya Miji na Vijiji. Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Serikali
Kuu zina wajibu wakutambua urithi wa asili na utamaduni na kuhifadhi kwa ajili
ya vizazi vijavyo mfano; mapango, wanyama, majengo ya kale, nakadhalika.
Nchini
Tanzania lengo hili bado halijapewa kipaumbele kwani maeneo mengi ya nchi
yamejengwa pasipo kufuata utaratibu wa mipango miji, nyumba zimebanana kiasi
cha kutoruhusu hata barabara za mitaa kupita na kufanya utoaji huduma muhimu
kama zima moto kushindwa kuwafikia wananchi kwa ufanisi pindi majanga ya moto
yanapotokea. Kwa uzoefu wangu na kwa maono yangu binafsi, ni mji wa Dodoma
pekee ambao umejitahidi kupangiliwa vizuri ukilinganisha na miji mingine.
Lakini
pia suala la uwiano wa huduma za kijamii kati ya sehemu ya mijini na vijijini
bado limeendelea kuwa changamoto kwani hakuna uwiano sawa wa upatikanaji wa
huduma hizo.
Matumizi
na Uzalishaji wenye Uwajibikaji
Lengo
hili linalenga kuhakikisha kunakuwepo na mifumo endelevu ya utumiaji na
uzalishaji wa rasilimali. Linasisitiza pia juu ya kupunguza kiasi kikubwa cha
taka kupitia mifumo endelevu ya kuzuia, kupunguza, na kuzichakata tena kwa
matumizi mengine. Suala la kupunguza upotevu wa chakula unaosababishwa na njia
mbaya za uzalishaji na usambazaji, ikiwa ni pamoja na hasara baada ya mavuno
pia limepewa msisitizo wa kutosha.
Linasisitiza
pia juu ya kuhakikisha manunuzi ya umma yanakuwa endelevu kulingana na sera na
vipaumbele vya kitaifa. Suala la uanzishwaji wa zana za kusimamia matokeo
chanya ya maendeleo endelevu kwaajili ya utalii ambao unazalisha ajira na
kuhamasisha utamaduni na bidhaa za ndani pia limepewa uzito wake.
Katika
kutekeleza lengo hili, nchi ya Tanzania imefaulu kwa kiasi chake hasa katika
kusimamia rasilimali zake kama madini. Kumetungwa sheria zinazosimamia
uzalishaji wa madinni ambao una manufaa kwa taifa. Suala la uzuiaji taka pia
halijaachwa nyuma, jitihada mbalimbali zimekuwa zikioneshwa na serikali katika
kupambana na uzalishaji taka nchini.
Kuchukua
Hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabia Nchi
Lengo
hili linalenga kuhakikisha nchi zote duniani zinachukua hatua za haraka
kupambana na mabadiliko ya hali ya nchi pamoja na athari zake. Limekusudia
kuimarisha uwezo wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja
na majanga yote katika nchi zote za ulimwengu.
Linalenga
pia kuboresha elimu na kuhamasisha watu pamoja na taasisi mbalimbali kupunguza
kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na njia za kukabiliana na
mabadiliko hayo kwa kutoa tahadhari kabla ya kutokea.
Linadhamiria
pia kukuza utaratibu wa kuongeza uwezo wa mipango na usimamizi wa hali ya hewa
inayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi ambazo zinaendelea kukua
na nchi ndogo za visiwa vinavyoendelea, huku msisitizo ukiwa kwa kundi la wanawake,
vijana na jamii zilizotengwa.
Suala
la kuingiza kwenye sera za nchi na mipango mbalimbali hatua zote zinazotakiwa
kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi pia linapewa msisitizo katika lengo
hili.
Nchini
Tanzania hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kudhibiti mabadiliko ya tabia
ya nchi ikiwa ni pamoja na kuhimiza zoezi la upandaji miti katika maeneo
mbalimbali ya nchi kama moja ya hatua katika kutekeleza lengo hili.
Licha
ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kupambana na mabadiliko
ya tabia ya nchi, nguvu zaidi bado zinahitajika ikiwa pamoja na kutoa elimu ya
mazingira kwa wananchi dhidi ya athari ya ukataji miti ovyo ambayo ni moja ya
sababu zinazopelekea mabadiliko ya tabia ya nchi kama ukame kutokea.
Kuendeleza
Uhai katika Maji
Lengo
hili linahimiza juu ya kuhifadhi na kutumia kwa njia endelevu malighafi za
baharini kwa ajili ya maendeleo endelevu. Limedhamiria kufikia mwaka 2025,
kunakuwa na matokeo chanya katika kuzuia na kupunguza kwa kiasi kikubwa
uchafuzi wa kila aina unaofanywa baharini ikiwa ni matokeo ya shughuli
mbalimbali za binadamu zinazoendelea kwenye fukwe za bahari.
Lina
lenga pia kufikia mwaka 2020, kuwe na matokeo chanya katika kuhifadhi angalau
asilimia 10 ya maeneo ya pwani na bahari, kulingana na sheria za kitaifa na
kimataifa juu ya usimamizi wa bahari. Usimamizi wa shughuli za uvuvi na kuzuia
uvuvi haramu pia ni miongoni mwa mambo yanayopewa uzito katika lengo hili la 14.
Nchini
Tanzania kumekuwa na jihada za kulizisha katika kutekeleza lengo hili.
Kumetungwa sheria mbalimbali za kulinda, kuifadhi, na kuendeleza viumbe vya
baharini na ziwani. Uvuvi haramu umekuwa ukipigwa vita, huku hatua stahiki
zikichukuliwa ikiwa ni pamoja na uchomaji nyavu zisizostahili.
Licha
ya matokeo chanya katika kutekeleza lengo hili, changamoto mbalimbali
zimeendelea kuwepo ikiwa ni pamoja na shughuli zenye kuhatarisha uhai wa viumbe
vya baharini kwenye maeneo ya ufukwe, uvuvi wa kutumia sumu, na kadhalika.
Kulinda
Uhai katika Ardhi
Lengo
hili linalenga kulinda uhai katika ardhi na baionuwai. Linasisitiza juu ya
kulinda na kurejesha katika hali ya awali mifumo ya mazingira ya nchi kavu,
huku kukiwa na udhibiti wa uharibifu wa misitu kwa njia endelevu, bila kusahau
kupambana na hali ya nchi kugeuka jangwa.
Linatia
mkazo pia katika kukomesha uharibifu wa ardhi na kupiga vita vitendo vyote
vinavyosababisha upotevu wa wanayama na mimea anuwai.
Serikali
na wadau wote wanalojukumu la kuhamasisha jamii juu ya ushiriki wao katika
kulinda, kusimamia maliasili za nchi hii kwa kuhakikisha unakuwepo ulinzi
shirikishi wa kuwalinda wanyama wetu dhidi ya majangiri.
Serikali
imepiga hatua kubwa katika kulinda maliasili zote ikiwemo wanyamapori hapa
nchini. Licha ya hatua kubwa hizo kumeendelea kuripotiwa vitendo vya ujangiri
katika baadhi ya maeneo, huku watu mbalimbali wakiendelea kukamatwa wakiwa na
nyara za serikali kama pembe za ndovu na meno ya tembo. Baadhi ya wanyamapori
wameendelea kupoteza maisha kwa kugongwa na magari hasa nyakati za usiku kwenye
hifadhi ambazo zimepitiwa na barabara.
Ni
jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda maliasili zetu kwa maendeleo ya kizazi
cha sasa na cha baadae.
Amani,
Haki na Taasisi Madhubuti
Lengo
hili limedhamiria kuendeleza jamii jumuishi na yenye amani kwa ajili ya
maendeleo endelevu, huku ikitoa haki kwa wote na kujenga taasisi imara zenye
kuwajibika katika nyanja zote. Linahimiza kudumisha usalama wa wananchi (raia)
ambao unategemea sana uwepo wa taasisi zenye ufanisi, zenye kuwajibika, na
zenye kuhusisha watu wote katika viwango vyote.
Serikali
inalojukumu lakuhakikisha kunakuwa na utawala bora, utawala wa kufuata sheria,
demokrasia, na haki inatolewa kwa wote bila upendeleo wowote ule. Inaowajibu
pia wa wakuonesha ufanisi na uwajibikaji kwa wananchi wake kwa kuhakikisha
inapambana na rushwa, na kuongeza uhuru wa wananchi kupata taarifa.
Licha
ya kufanya vizuri katika kusimamia utawala bora na demokrasia nchini, bado
kumekuwepo na malalamiko ya baadhi ya watumishi na watendaji wa serikali
kutokufuata utawala wa sheria, ni wakati sasa wahusika wajitathimini na
kufikiria upya namna nzuri ya kuweza kufanikisha lengo hili kwa kuhakikisha
wanafuata utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.
Katika
kupambana na rushwa serikali imefanya vizuri sana. Tumeshuhudia mafisadi
wakifikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua stahiki. Licha ya
kufanya vizuri katika kupambana na rushwa, vitendo vya rushwa vimeendelea
kuripotiwa sehemu nyingi za nchi, hivyo naiomba serikali kuendeleza vita hii
maana haki haiwezi kupatikana endapo kuna utitiri wa rushwa, na rushwa siku
zote ni adui wa haki.
Baadhi
ya kesi mahakamani zimeendelea kuchukua muda mrefu bila kusikilizwa huku
watuhumiwa wakiendelea kusota rumande na mahabusu bila sababu za msingi.
Watuhumiwa pia wameendelea kunyimwa dhamana hata kwa makosa ambayo yanastahili
dhamana. Mabambiko ya kesi yameendelea kuwepo licha ya kupungua kwa kiasi
kikubwa ukilinganisha na siku za nyuma.
Matukio
ya watu kutekwa, kupotea katika mazingira ya kutatanisha, na baadhi ya miili ya
watu kuokotwa wakiwa wamekufa, ni miongoni mwa mambo yanayoenda kinyume na
lengo hili. Ni wajibu wa seriklia na raia wote kuhakikisha wanakomesha jambo
hili. Serikali ifuatilie matukio haya, na wananchi watoe ushirikiano kwa
serikali kwa kutoa taarifa za matukio haya polisi kabla na baada ya kutokea.
Ushirikiano
ili Kufanikisha Malengo
Kama
ilivyo usemi usemao ‘umoja ni nguvu,
utengano ni udhaifu’, lengo hili linazitaka nchi zote na wadau wote
kuendeleza ubia katika ngazi zote ili kuweza kufanikisha Malengo ya Maendeleo
Endelevu. Linasisitiza juu ya kuimarisha njia za utekelezaji kwa kuunganisha
nguvu na ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu.
Linahimiza
juu ya ushirikiano katika masuala ya kifedha, teknolojia, biashara, masuala ya
kisera, na masuala ya kuzijengea uwezo nchi maskini kuweza kutekeleza mipango
yake. Linalenga kuimarisha uwezo wa nchi katika kusimamia na kukusanya mapato
ya ndani, huku ikizitaka nchi zilizoendelea kutoa misaada kwa nchi
zinazoendelea (maskini) katika kufanikisha malengo yake.
Tumeona
serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wa kimataifa na kitaifa katika
kutekeleza malengo haya. Licha ya jitihada hizi kufanyika, mimi binafsi naona
haitoshi hivyo naendelea kuomba ushirikiano zaidi toka pande nne za dunia
katika kufanikisha malengo haya. Lazima tuhakikishe dunia inakuwa sehemu salama
kwa binadamu kuishi huku akifurahia utu wake.
Serikali
kuanzia ngazi ya serikali za mitaa hadi serikali kuu zinaowajibu wa kuhakikisha
upatikanaji wa rasilimali, teknolojia pamoja na maarifa ya kutekeleza malengo yote
endelevu. Hii ikiwa ni pamoja na serikali kuhakikisha inatenga fedha za kutosha
kwa kila wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi maana tunaamini wizara
zote zinatekeleza malengo haya.
HITIMISHO
Ni
matumaini yangu kuwa baada ya kusoma makala hii fupi, kila mmoja wetu atafanya
jitihada za kuhakikisha malengo haya 17 yanatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Malengo yote yanatekelezeka, tuungane kwa pamoja kuyatekeleza.
No comments:
Post a Comment