SURA YA NNE
MALEZI
Majukumu ya Mzazi, Mlezi, Meneja au
Mzazi Mlezi
(i) Mlezi wa makazi yaliyoidhinishwa
kwa ajili ya malezi; au meneja wa taasisi au mlezi aliyepewa majukumu ya kumlea
mtoto; atakuwa na majukumu ya mzazi kwa mtoto wakati wote mtoto anapokuwa chini
ya uangalizi wake.
(ii) Mawasiliano ya mtoto na wazazi,
ndugu au marafiki yanaruhusiwa wakati mtoto yuko katika makazi yaliyoidhinishwa,
taasisi au kwa mlezi. Kama mawasiliano hayo hayatampa mtoto furaha na amani,
mawasiliano yatasitishwa.
(iii) Mlezi au meneja wa makazi
yaliyoidhinishwa au taasisi au mlezi aliyekabidhiwa jukumu la kumlea mtoto,
atahakikisha kuwa anaangalia kwa makini maendeleo ya mtoto, hususani afya yake
na elimu kwa kipindi chote.
(iv) Mlezi au meneja wa makazi
yaliyoidhinishwa au taasisi, atawasiliana na wazazi au walezi wa mtoto kuwapa
taarifa ya maendeleo ya mtoto. Kwa kupitia Ofisa wa Ustawi wa Jamii, mlezi au
meneja wa makazi atapanga muda wa kurudi nyumbani kwa majaribio mapema
iwezekanavyo.
(v) Ofisa wa Ustawi wa Jamii anatakiwa
kumtembelea mtoto anapokuwa nyumbani kwa kipindi cha majaribio. Pia atapanga
mipango ya baadaye ya mtoto kwa kushauriana na meneja, mlezi au wazazi walezi.
Kipidi cha majaribio ni kipindi
ambacho mtoto anarudishwa nyumbani kuangalia kama mazingira yaliyofanya
aondolewe na kupelekwa kwenye makazi yaliyoidhinishwa yamebadilika kiasi cha kumfanya
mtoto aishi kwa amani au furaha.
Amri ya Kizuizi
Amri ya kizuizi hutolewa kwa nini?
(i) Mahakama ya Watoto inaweza kutoa
amri ya kumzuia mtu asiwe na mawasiliano na mtoto au na mtu atakayepewa jukumu
la kumlea mtoto. Kizuizi hiki kitategemea mwenendo wa tabia ya mtu aliyeshindwa
kutimiza majukumu ya usimamizi na matunzo ya mtoto.
(ii) Kabla ya kuweka amri ya kizuizi,
mahakama inatakiwa ijiridhishe kuwa amri hiyo ni ya muhimu. Amri ya kizuizi
itawekwa kwa lengo la kumlinda mtoto na ustawi wake.
(iii) Mahakama inaweza kutamka muda
ambao amri ya kizuizi itadumu.
Utekelezaji wa Amri ya Kizuizi
(i) Mahakama ya Watoto inaweza
ikabadili au kuondoa amri ya kizuizi. Hili litafanyika kama mtu aliyetajwa katika
amri ya kizuizi au mtoto anayehusika ataomba amri iondolewe au ibadilishwe.
(ii) Iwapo Ofisa wa Ustawi wa Jamii
anaamini au anatuhumu kuwa mtoto anapata mateso au anaweza kupata madhara
makubwa, Mahakama inaweza kutoa amri kwa Ofisa wa Ustawi wa Jamii ya kufanya
upekuzi. Pia mahakama itatoa amri ya kumtoa mtoto kulingana na mwenendo wa maombi
ya amri ya matunzo au amri ya usimamizi.
Ofisa wa Ustawi wa Jamii ataweza
kuingia katika nyumba iliyotajwa katika amri hiyo na kufanya upekuzi, kumtoa mtoto
na kumpeleka mahali penye usalama. Mtoto atatolewa na Ofisa wa Ustawi wa Jamii,
akiwa au hata asipokuwa na polisi.
(iii) Mtoto aliyetolewa kwa
kutekeleza amri ya mahakama ya kufanya upekuzi na kumtoa, atapelekwa mahakamani
ndani ya kipindi cha siku saba baada ya kutolewa.
(iv) Katika kipindi cha siku saba
baada ya kumtoa mtoto kwa amri ya mahakama, Ofisa wa Ustawi wa Jamii atampeleka
mtoto mahakamani akiwa na taarifa inayozingatia matakwa ya mtoto.
(v) Pale mtoto atakapokuwa chini ya
malezi ya wazazi wake, walezi au mtu yeyote anayeishi na mtoto, mtu huyo atataarifiwa
mapema iwezekanavyo. Pia ataruhusiwa kuwa na mawasiliano na mtoto isipokuwa kama
mawasiliano hayo yatamkosesha mtoto furaha na amani.
(vi) Mtu yeyote anayekiuka amri ya
kizuizi atakuwa anatenda kosa. Akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini si
chini ya shilingi laki tano au kifungo cha miezi mitatu au vyote kwa pamoja.
Kumtoa mtoto pasipokuwa na Mamlaka
(i) Mtu yeyote atakuwa anatenda kosa
kama atamtoa mtoto ambaye yuko chini ya uangalizi wa malezi au mahali pa usalama,
bila sababu ya msingi. Au akifanya hivyo bila kuwa na mamlaka au kibali cha mtu
anayemtunza mtoto. Akitiwa hatiani atalipa faini si chini ya shilingi laki moja
au kifungo kisichozidi miezi mitatu au vyote kwa pamoja.
(ii) Ofisa wa Ustawi wa Jamii, baada
ya kufanya uchunguzi, atamrudisha mtoto mahali pa usalama kama kunahitajika kufanya
hivyo.
Masharti ya Malezi
(i) Ofisa wa Ustawi wa Jamii, kwa
kushirikiana na mlezi au meneja wa makazi au taasisi yaliyoidhinishwa anaweza
kutoa mapendekezo kwa Kamishna kumuweka mtoto chini ya mtu anayetaka kuwa
mlezi.
Hii litafanywa badala ya kumpeleka
mtoto chini ya usimamizi wa makazi au taasisi iliyoidhinishwa.
(ii) Mtu anayetaka kuwa mlezi wa
mtoto atapeleka maombi kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii.
(iii) Baada ya kupokea maombi,
Kamishna, ataangalia maombi kulingana na mapendekezo yaliyofanywa na Ofisa wa
Ustawi wa Jamii, mlezi na meneja.
(iv) Kamishna akiridhika kuwa mlezi
mwombaji anaweza kumlea na kumtunza mtoto, na kuzingatia ustawi wake, atatoa
kibali cha mtoto kuwa chini ya malezi ya mwombaji.
Amri ya Malezi na Kuasili
Mtoto ambaye mzazi au mlezi wake hana
nia ya kumlea anaweza kufanyiwa nini ?
(i) Mtoto ambaye yuko chini ya amri
ya matunzo au usimamizi, ambaye mzazi wake, mlezi au ndugu yake, haonyeshi nia
ya kudumisha furaha na amani ya mtoto, anaweza kupendekezwa aasiliwe. Mtoto ataasiliwa
kwa mlezi au mahali pa malezi chini ya malezi ya mlezi wa makazi
yaliyoidhinishwa.
(ii) Maombi ya amri ya malezi au
usimamizi yanaweza kufanywa katika mazingira yafuatayo:
(a) Baada ya jitihada mbalimbali za
kumsaidia mtoto kufanywa na kushindikana;
(b) Madhara makubwa anayopata mtoto
au anayoweza kupata yanaweza kuepukwa kwa kumuondoa mtoto mahali anapoishi.
(iii) Iwapo mtoto ataendelea kuishi
mahali alipo, anaweza akapatwa na hatari kubwa.
Lengo la Amri ya Malezi
(i) Amri ya matunzo au
usimamizi hutolewa kwa sababu gani ?
(a) Kumtoa mtoto kwenye mazingira
ambayo anateseka au anaweza kupata madhara
makubwa.
(b) Kumsaidia mtoto na wale anaoishi
nao au anapenda kuishi nao; na
(c) Kuchunguza mazingira
yaliyosababisha kutoa amri na kuchukua hatua ili kupata suluhu au kuondoa tatizo
ili kuhakikisha mtoto anarudi kwenye jamii.
(ii) Ofisa wa Ustawi wa Jamii ataomba
amri ya matunzo au usimamizi ifanyiwe uhakiki walao mara moja kila mwaka.
No comments:
Post a Comment