Wednesday, June 27, 2018

TUTEKELEZE MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGs)

Mnamo Septemba 25, 2015, Malengo ya Maendeleo Endelevu, yaani Sustainable Development Goals (SDGs) yalipitishwa na nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) katika mkutano maalam wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jijini New York nchini Marekani.

Malengo haya yalianza kutumika rasmi tarehe 1 Januari, 2016.        

Basi tupate fursa ya kuyatazama malengo haya kwa undani wake.


Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ni nini?
Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ni seti ya malengo 17 ya ulimwengu ambayo yamedhamiria kuubadilisha ulimwengu kutoka katika hali yake ya sasa ambayo imejaa umaskini wa kutisha, changamoto ya njaa, mabadiliko ya tabia ya nchi, uhaba na ubovu wa huduma za msingi za jamii kama vile elimu na afya, machafuko na ghasia, uchumi husio jumuishi, na matatizo ya ajira na kazi zisizo za staha, kwenda kwenye ulimwengu ambao utakuwa hauna aina zote za umaskini, ulimwengu wenye chakula cha kutosha, huduma nzuri za afya, elimu, maji, nishati, miundombinu ya usafirishaji, usawa wa kijinsia, na haki na usawa kwa jamii.

Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu
Orodha ya malengo 17 ya maendeleo endelevu ni pamoja na: 1. kutokomeza umaskini, 2. kukomesha njaa, 3. afya njema na ustawi, 4. elimu bora, 5. usawa wa kijinsia, 6. maji salama na usafi, 7. nishati mbadala kwa gharama nafuu, 8. kazi zenye staha na ukuzaji uchumi, 9. viwanda, ubunifu na miundombinu, 10. kupunguza tofauti, 11. miji na jamii endelevu, 12. matumizi na uzalishaji wenye uwajibikaji, 13. kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi, 14. kuendeleza uhai katika maji, 15. kulinda uhai katika ardhi, 16. amani, haki na taasisi madhubuti, na 17. ushirikiano ili kufanikisha malengo.

Katika sehemu hii ya kwanza, tutaangalia Lengo Namba Moja (No.1) hadi  Lengo Namba Tano (No.5).

Kutokomeza Umaskini
Hadi kufikia mwaka 2030 Umoja wa Mataifa umedhamiria kuwa umaskini wa aina zote katika kila mahali unatokomezwa kabisa na kuhakikisha kuwa watu waishio kwenye umaskini wanajiongezea kipato na kupata huduma za msingi, pamoja na kuepukana na majanga mbalimbali.

Kwa mantiki hiyo basi, ni jukumu la serikali na wadau wote wanaohusika kuhakikisha kuwa wanatokomeza umaskini ulioshamiri kwa watu wote hususani wale wanaoishi chini ya dola moja ya kimarekani kwa siku ambao idadi yao inakadiriwa kuwa robo ya jumla ya watanzania wote.

Serikali na wadau wote wanaohusika wanalojukumu pia la kuhakikisha wanawatambua wananchi wanaoishi katika hali ya umaskini, ili kuelekeza rasilimali na huduma mbalimbali za kijamii ili kuwasaidia kuepukana na hali hiyo. Zoezi hilo likienda sanjari na kuwajengea uwezo wa kiuchumi kwa kuwapatia huduma za kifedha na mikopo ili iwasaidie kujiinua kiuchumi.

Ni ukweli husiopingika kuwa wananchi wengi bado wanaishi katika hali ya umaskini wa kutupwa. Kwa uzoefu wangu binafsi na kwa kupitia ripoti mbalimbali, mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Dodoma, Lindi, Mtwara na Pwani, ni miongoni mwa mikoa ambayo wananchi wake wanaishi kwenye hali ya umaskini unaotia huruma. Ni wakati sasa kwa mamlaka zinazohusika kuitizama mikoa hii ili kutekeleza lengo hili na kutokomeza umaskini kwa vitendo.

Kukomesha Njaa
 
Lengo hili linadhamiria kutokomeza na kumaliza kabisa njaa kwa kusisitiza upatikanaji wa chakula cha uhakika, utolewaji wa lishe bora, huku likihimiza kukuza kilimo endelevu. Linaendelea kubainisha njaa kama tatizo linalopaswa kuondolewa kwa kushughulikiwa kikamilifu ili kuhakikisha kila kaya inakuwa na uhakika wa kupata chakula salama na cha kutosha ambacho kina virutubisho vyote.

Lengo hili linadhamiria pia hadi kufikia mwaka 2030, kilimo kiwe kimeboreshwa kwa kuhakikisha wakulima wanatumia zana za kisasa na bora, urutubishaji wa ardhi inayotumika kwaajili ya kilimo, na kuongeza uwezo wa wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na majanga kama vile; mafuriko, ukame, na ndege waharibifu. Hii itasaidia kukuza uzalishaji wa mazao na hivyo kutokomeza kabisa balaa la njaa.

Ili kuhakikisha lengo hili linafanikiwa kikamilifu, ni wajibu wa serikali na mamlaka zote zinazohusika kuhakikisha wanaweka jitihada kwenye kuongeza uzalishaji katika kilimo kwa kuhakikisha zana za kilimo ikiwa ni pamoja na pembejeo za kilimo, na viuatilifu vya wadudu wanaoshambulia mazao zinapatika kwa urahisi zaidi kwa wakulima kote nchini.

Ni ukweli husiopingika kuwa, sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji imekuwa haipewi kipaumbele cha dhati na watawala katika nchi hii. Kumekuwepo na sera nyingi zenye dhamira yakuhimiza shughuli za kilimo, lakini sera hizo zote hazikuweza kufanikiwa kwa kiasi kilichotarajiwa. Sera ya hivi karibuni ya ‘Kilimo Kwanza’ chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ilileta matumaini kwa wakulima wengi, lakini matumaini yao yalizimika ghafla kama mshumaa, na hivyo mpaka sasa hakuna msisitizo wala matumaini mapya katika kilimo.

Nipende kushauri jambo katika kuboresha sekta ya kilimo ambayo ndiyo sekta pekee itakayo tuhakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha; ni wakati sasa wa mawaziri wanaokabidhiwa kusimamia wizara hii wawe ni wakulima kwa asili, nadhani hii itasaidia katika kuweka msisitizo wa kilimo hapa nchini. Pia napendekeza yatengwe maeneo maalumu kwaajili ya kilimo na yawe chini ya usimamizi wa serikali, vijana waliomaliza mafunzo yao kwenye masuala ya kilimo wakabidhiwe jukumu la uzalishaji mazao ya chakula katika maeneo haya. Hii naamini itasaidia katika kutekelza lengo hili kwa vitendo zaidi.

Afya Njema na Ustawi
 
Lengo hili limedhamiria kuhakikisha kuwa watu wana afya njema na ustawi wa watu katika umri na rika zote. Linatia msisitizo katika kuwawezesha watu kuishi maisha yenye afya bora ili kuongeza umri wa kuishi kwa watu wa umri na rika zote ifikapo mwaka 2030.

Hili kuhakikisha lengo hili linafikiwa kikamilifu, Umoja wa Mataifa umetia mkazo katika kupunguza vifo vya watoto na wakinamama wakati wa kujifungua kunakosababishwa na kukosekana huduma na vifaa bora vya kujifungulia, na kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ambao wengi wao wamekuwa wakipoteza maisha kwa ugonjwa wa malaria ambao umekuwa sugu barani Afrika.

Vile vile lengo hili linalenga kutokomeza maambukizi ya UKIMWI na VVU, magonjwa mbalimbali kama kifua kikuu, kisukari, shinikizo la damu, malaria, vikope, nimonia, kichocho, kipindupindu, homa ya matumbo, pia magonjwa mengine yanayoambukiza kama magonjwa ya zinaa ambayo yamekuwa yakisumbua kwa kiasi kikubwa.

Lengo hili pia limedhamiria kupunguza vifo na ulemavu unaosababishwa na ajali za barabarani, kupunguza magonjwa na vifo vinavyotokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na madawa yenye sumu kuchanganyikana na hewa safi, maji na udongo vitu ambavyo vinatumiwa na binadamu kwaajili ya ustawi wa maisha yao. Bila kusahau kuhakikisha elimu na stadi za huduma ya afya ya uzazi kwa wananchi zinapatikana kwa urahisi zaidi.

Mengi yamefanywa na serikali katika kutekeleza lengo hili, lakini bado changamoto ni nyingi hasa maeneo ya vijijini ambako huduma za afya bado zinapatikana kwa kusua sua. Baadhi ya vijiji havina kabisa zahanati, huku baadhi ya mikoa ikikosa hospitali za rufaa. Upatikanaji wa madawa bado ni mtihani mkubwa sana, huduma kwa mama mjamzito na mtoto zinatolewa lakini si kwa kiasi kinachotakiwa. Baadhi ya maeneo wazee wamekuwa bado wakitozwa pesa ili kupata huduma ya afya ambayo inapaswa waipate bure pasipo malipo yoyote.

Baadhi ya maeneo wamama wamekuwa wakijifungulia nyumbani, na wengine vichakani wakiwa njiani kuelekea hospitalini kutokana na umbali wa sehemu huduma za afya zinakopatikana. Vifo vya wakinamama na watoto wakati wa kujifungua vimepungua ila havijaisha kabisa, idadi ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wanaokufa kwa malaria imepungua japo nayo haijaisha kabisa.
Utekelezaji wa lengo hili unahitaji mikakati endelevu ambayo inapaswa kuwashirikisha watanzania wote. Lazima kuwepo usimamizi makini kuanzia ngazi ya taifa hadi serikali za mitaa. Wadau mbalimbali pia wajitokeze kusaidia sekta ya afya nchini kwa kujitolea kujenga vituo vya afya kwenye vijiji ambavyo havina huduma hii, pia wasaidie upatikanaji wa madawa katika hospitali na zahanati zote nchini.

Serikali pia ihakikishe inazalisha wataalamu wa kutosha wa kuhudumu katika sekta hii maana kumekuwa kukiripotiwa upungufu wa wataalamu (specialists) katika nyanja mbalimbali za afya. Pia ihakikishe inadhibiti madaktari feki ambao wamekuwa wakijipenyeza katika baadhi ya mahospitali kwani suala hili linahatarisha usalama na uhai wa mgonjwa endapo atahudumiwa na daktari feki asiyekuwa na ujuzi wa kitabibu.

Elimu Bora
 
Lengo hili linalenga kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora na jumuishi, inayozingatia usawa na kutoa fursa kwa wote kujiendeleza. Linasisitiza kuwezesha kila mtu kusoma, kujifunza na kuhakikisha kwamba binadamu wote wanafikia vipawa vyao kikamilifu.

Lengo hili linalenga kupunguza idadi ya watu ambao hawajui kusoma na kuandika duniani huku likisisitiza kuboreshwa kwa mazingira ya kutolea elimu, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa walimu wa kutosha, vitabu vya kutosha vinavyokidhi vigezo, miundombinu bora kama madarasa, meza na madawati.

Vile vile linasisitiza juu ya utoaji fursa ya elimu kwa watu wote isiyokuwa na ubaguzi kwa watu wenye ulemavu, huku likidhamiria kuongeza idadi ya vijana na watu wazima wenye ujuzi pamoja na ufundi stadi kwa ajili ya ajira, kazi zenye heshima na ujasiriamali.

Nchini Tanzania lengo hili linaendelea kutekelezwa kwa kasi ambayo tunaweza kusema ni ya kulizisha. Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali iliyopo madarakani kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa wananchi wake ili kuwajengea uwezo wa kupambana na umaskini ambao umekuwa tatizo kwa taifa.

Katika kuhakikisha lengo hili linatekelezwa kwa vitendo, serikali imekuja na sera ya elimu bure ambayo inatoa fursa sawa kwa watoto wa maskini na matajiri kupata elimu sawa, tofauti na hapo zamani ambapo watoto wengi wa maskini walishindwa kupata fursa hii kwa kukosa mahitaji muhimu ya kishule ikiwa ni pamoja na ada, michango ya madawati na taaluma, michango ya walinzi, na hata michango kwaajili ya ujenzi wa maabara.

Tumeshuhudia pia serikali ikiendesha kampeni mbalimbali kwaajili ya upatikanaji madawati, meza na viti, ambavyo vimekuwa vikipelekwa mashuleni kwaajili ya kurahisisha zoezi la ufundishwaji kwa kuwawezesha wanafunzi kujifunza wakiwa wamekaa na kustarehe kabisa. Suala la upatikanaji wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia pia limefanyiwa kazi licha ya kuwa bado kuna kasoro mbalimbali katika baadhi ya masomo.

Mkoa wa Dar es Salaam unaweza kuwa mkoa wa mfano kwa Tanzania kwa kuonesha jitihada zake kwa vitendo katika kutekeleza lengo hili. Tumeshuhudia uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na wadau wa elimu wakifanikisha upatikanaji wa meza, viti, na madawati kwa wanafunzi wa mkoa huo, huku miundombinu kama ofisi na nyumba za walimu zikijengwa tena kwa hadhi juu.

Licha ya mafanikio hayo machache, changamoto katika sekta ya elimu bado ni nyingi na zinahitaji ufumbuzi wa haraka ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 lengo hili liwe limefikiwa kwa asilimia mia moja. Walimu wameendelea kulalamikia mishahara midogo, jambo linaloshusha morali ya ufundishaji kwa walimu hao. Walimu wa masomo ya sayansi kwa shule za sekondari bado hawatoshi, huku wale wa masomo ya sanaa (arts) wakisubiri ajira kwa takribani miaka miwili sasa bila kuajiriwa. 

Usawa wa Jinsia
 
Lengo hili linalenga kufanikisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na wasichana wote. Linakusudia kutokomeza ukatili wa aina zote dhidi ya wanawake na wasichana kwa kuhakikisha wanapata fursa sawa katika umiliki wa rasilimali za kiuchumi kama vile ardhi, nyumba, na hata magari.

Lengo hili linasisitiza hadi kufikia mwaka 2030 kusiwe na vitendo vya kikatili kwa wanawake na wasichana ambavyo vimekuwa vikisababishwa na baadhi ya tamaduni ovu ambazo zimekuwa zikikumbatiwa na baadhi ya jamii hapa duniani, ikiwemo Tanzania. Vitendo kama ukeketaji na ndoa za utotoni kwa watoto wa kike ni miongoni mwa vitendo vinavyopigwa vita na Umoja wa Mataifa kupitia lengo hili.

Lengo hili pia linakusudia kutoa fursa za elimu, uongozi, na ajira kwa wasichana na wanawake kama ilivyo kwa wavulana na wanaume. Kwa kipindi kirefu sasa, kundi la wasichana na wanawake limekuwa likibaguliwa katika masuala ya elimu, uongozi, na ajira, ambapo fursa nyingi zimekuwa zikitolewa kwa wanaume na wavulana zaidi. Lengo hili limekuja kama mwarobaini wa kutibu suala hili ambalo tunaweza kuliita ni kansa sasa.

Kwa upande wake nchi ya Tanzania imejitahidi kwa kiwango chake katika kutekelza lengo hili. Idadi ya wasichana kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu ni kubwa ukilinganisha na ilivyokuwa hapo awali. Idara nyingi za serikali na binafsi pia zimeajiri wanawake wa kutosha. Bila kusahau baraza la mawaziri nalo limejumuisha wanawake, achilia mbali wakuu wa mikoa na wilaya ambao nao pia kuna wanawake ndani yake.

Mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kama Children’s Dignity Forum (CDF), UNICEF Tanzania, Save the Children, WHO, na mengine mengi yamekuwa yakipinga vikali vitendo vya kikatili dhidi ya watoto wa kike ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni na ukeketaji. Wizara ya Afya pia imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu juu ya athari ya ndoa (mimba) za utotoni pamoja na ukeketaji.

Licha ya jitihada hizo zote, msisitizo na mkazo zaidi unatakiwa kuendelea kutolewa katika kukemea vitendo vya kikatili dhidi ya mtoto wa kike ambavyo vimeendelea kuripotiwa katika baadhi ya mikoa hapa nchini. 

Baada ya kuyatazama malengo haya matano ya mwanzo (Lengo No.1 hadi No.5), Je utekelezaji wake ukoje katika eneo lako? Kuna jitihada zozote ambazo zinafanywa na serikali kutekeleza malengo haya?, Je wewe binafsi upi ni mchango wako katika kutekeleza Malengo haya?

1 comment:

  1. asante kwa elimu hii, ata mimi nasikiaga tu malengo ya dunia lakn sikujua ni nini

    ReplyDelete

FAHAMU KUHUSU MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGs)


SHULE INAYOTOA MICHEZO KAMA HII INAFAA KWA MZAZI NA MLEZI KUPELEKA MTOTO WAKE