Sheria
hii ni sehemu ya utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ambayo imekuwa ikilenga
kutetea na kupigania haki na ustawi wa mtoto katika kila kona ya ulimwengu.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na: Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto,
yaani The UN Convention on the Rights of the Child (CRC), na Mkataba wa Afrika
wa Haki na Ustawi wa Mtoto, yaani The African Charter on the Rights and Welfare
of the Child.
Moja
ya dhamira kuu ya sheria hii ni kuimarisha ulinzi kwa mtoto kwa kuhakikisha
kuwa hakuna aina yoyote ya ukatili unaofanywa dhidi ya mtoto, vilevile
kuhakikisha kuwa hakuna unyanyasaji na ubaguzi wowote unaofanywa dhidi ya
mtoto.
Licha
ya sheria hii kuwepo tangu mwaka 2009, ni watanzania wachache wanaofahamu juu
ya uwepo wa sheria hii, na baadhi yao wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya ukatili
watoto kwa kisingizio cha kutokufahamu sheria inayomlinda mtoto. Wengine pia
wamekuwa wakidai wanashindwa kuelewa maana halisi ya ‘ukatili dhidi ya watoto’.
Wapo
ambao wamekuwa wakihoji, ‘Je mtoto (mwanangu) kunisaidia kazi ni kitendo cha
ukatili?, Kumpa adhabu mtoto (mwanangu) anapokuwa amekosea ni kitendo cha
ukatili?, Je kumfanyia utamaduni binti yangu (ukeketaji) ni kitendo cha
ukatili?. Hayo ni baadhi tu ya maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa sana na
wazazi na walezi nchini Tanzania.
Ili
kuondoa mkanganyiko uliopo miongoni mwa watanzania, na katika kutimiza azima
yake ya kuhakikisha kuwa mtoto wa kitanzania (watoto wote duniani) analindwa,
Everybody Newz inakuletea elimu juu ya Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009.
Tutarejelea sheria yenyewe, na kwa kiasi kikubwa tutatumia tafsiri rahisi ya sheria
hiyo kama ilivyotolewa na HakiElimu, pamoja na marejeo mengine yanayohusu
Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009.
SURA YA KWANZA
UTANGULIZI
Hii ni Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
Sheria ya Mtoto inahusu nini?
Sheria hii ya mtoto inazungumzia:
- sheria za mtoto,
- haki za mtoto,
- kukuza, kulinda na kuhifadhi ustawi wa mtoto,
- masharti ya unasibishaji wa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa,
- masuala ya kulea, kuasili na uangalizi.
- Pia inatoa maelezo na masharti yanayohusu mtoto anapokuwa katika migogoro na sheria.
Sheria hii inatumika eneo lote la
Tanzania Bara kutetea masuala yote ya kuboresha, kulinda, na kuhifadhi ustawi
wa mtoto pamoja na haki zake.
(Sheria hii itatumika eneo lote la
Tanzania Bara. Sheria itatumika kutetea masuala yote ya kuboresha, kulinda na kuhifadhi
ustawi wa mtoto pamoja na haki zake. Sheria hii ya mtoto imetungwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Novemba 2009).
2
Dhana muhimu na maana zake
katika Sheria hii, dhana hizi muhimu
zitakuwa na maana zifuatazo:
Makazi yaliyoidhinishwa: maana yake ni makazi yenye kibali
ambapo mtoto anaweza kupewa huduma mbadala za malezi ya familia.
Shule iliyoidhinishwa: ina maana ya shule iliyoanzishwa
chini ya sheria hii ambapo watoto wanaweza kutunzwa na kupata elimu. Shule
iliyoidhinishwa inaweza ikawa mahali popote au ikawa taasisi iliyotamkwa chini ya
sheria hii.
Elimu ya Msingi: ina maana ya elimu rasmi
inayotolewa kwa mtoto kumpatia maarifa ya msingi na muhimu. Mtoto anaweza
kupatiwa elimu ya msingi wakati wowote itakapodhihirika kwamba mtoto anahitaji
maarifa ya msingi.
Kupotosha mtoto (Ukatili dhidi ya
mtoto): maana yake ni
kukiuka haki za mtoto kunakosababisha madhara ya mwili, maadili au hisia. Kwa
hiyo, kupotosha (ukatili dhidi ya mtoto) mtoto ni pamoja na kumpiga, kumtukana,
kumtenga, kumtelekeza, kumnajisi na kumnyonya kwa kumtumikisha. Mtoto anaweza kudhurika
kwa njia zote hizo wakati anapotendewa tendo asilolipenda.
Maendeleo ya mtoto: kuhusiana na ustawi wa mtoto, yaani
wakati ambapo mtoto anajifunza kwa kufurahia na kukua katika mazingira mazuri.
Kwa hiyo, maendeleo ya
mtoto ni mlolongo wa mabadiliko
ambayo mtoto anaweza kupata kimwili, kiakili, kihisia na kijamii. Maendeleo ya
mtoto hutokea wakati wote katika maisha yake kwa kadiri anavyohusiana na mazingira
yanayomzunguka, kama shule, nyumbani, michezoni na sehemu nyingine.
Mtoto mwenye ulemavu: ni mtoto ambaye ana mapungufu au udhaifu
wa muda mrefu au wa kudumu, wa mwili, akili, hisia au mfumo wa fahamu. Ni
ulemavu ambao unamzuia asiweze kushirikiana kikamilifu na wenzake. Kuna ulemavu
wa viungo vya mwili, wa akili, kama utindio wa ubongo, wa mfumo wa fahamu
mfano, uziwi au upofu.
Kamishna: ina maana ya Kamishna wa Ustawi wa Jamii.
Kamishna ni ofisa wa Serikali katika Wizara ya Wanawake, Watoto na Ustawi wa
Jamii.
Mahakama: ina maana ya:
(a) Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya
Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi au Mahakama Kuu.
(b) Kwa madhumuni ya kuasili,
Mahakama Kuu; na
(c) Kwa madhumuni ya uzawa, Mahakama
ya Watoto.
4
Fundistadi: ina maana ya mtu ambaye anafundisha na
kutoa maelekezo kwa mwanagenzi katika ufundi. Mwanagenzi ni mwanafunzi wa
ufundi.
Kituo cha kulea watoto wachanga: ni kituo kilichosajiliwa kwa
madhumuni ya kuwapokea na kuwalea watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wanaofikia
idadi si zaidi ya kumi wakati wa mchana, kwa malipo au pasipo malipo ya ada.
Familia: maana yake ni baba mzazi, mama mzazi
na watoto walioasiliwa au wa damu pamoja na ndugu wa karibu, ikihusisha babu,
bibi, wajomba, shangazi, binamu, wapwa ambao wanaishi katika kaya moja.
Mtu anayefaa: maana yake ni mtu mzima, mwenye uadilifu
na mwaminifu, aliye na akili timamu, ambaye si ndugu wa mtoto lakini ana uwezo
wa kulea mtoto. Huyu mtu awe amethibitishwa na Ofisa wa Ustawi wa Jamii kwamba
anaweza kutoa mahali pa kukaa na kuishi kwa ajili ya malezi ya mtoto.
Malezi au kukimu: maana yake ni kupata upendo, mafundisho
na maelekezo ya kawaida ili mtoto aishi vema, kwa kipindi cha muda mfupi.
Kukimu ni kupata mahitaji ya msingi ya chakula, mavazi, mahali pa kulala na
dawa mtoto anapougua. Huduma hii inaweza kutolewa kwa hiari na familia au mtu
binafsi ambaye hana udugu na mtoto ili kumpatia hifadhi na ulinzi.
5
Mlezi: maana yake ni mtu anayewajibika na
mwenendo wa maisha ya kila siku ya mtoto, lakini ambaye sio baba au mama mzazi.
Mlezi anakuwa ameteuliwa na mahakama kwa maandishi au kwa wasia ulioachwa na
mzazi au kwa amri ya mahakama. Mlezi anakuwa na mamlaka na wajibu wa kumlea mtoto
na kusimamia mali na haki za mtoto.
Kazi ya hatari: maana yake ni kazi yoyote
inayomfanya mtoto awe katika hatari ya kuumia kimwili au kiakili. Kwa mfano,
kazi kwenye machimbo au kazi ya kupigana vita.
Nyumbani: maana yake ni mahali panapojulikana anapoishi
mtoto. Nyumbani panaweza pasiwe mahali anapoishi baba na mama, au ndugu, lakini
pawe mahali ambapo mzazi au mlezi aliwahi kuishi na kujulikana kwamba aliishi
hapo. Kwa mfano, kama mzazi ametokea Mbeya na ana nyumba ya kuishi huko Mbeya,
nyumbani panaweza kuwa Mbeya hata kama mtoto anaishi naye hapa Dar es Salaam.
Isipokuwa kwamba:
(a) Kwa mzazi au mlezi mwenye makazi
ya kudumu zaidi ya sehemu moja, mzazi au mlezi huyu atachukuliwa kuwa anaishi pale
ambapo anapatambua kuwa ni makazi yake rasmi ya kudumu. Kwa mfano, mzazi aliye
na nyumba Dar es Salaam na Mbeya, anaweza kutambua Dar es Salaam kama makazi ya
kudumu. Hapo patakuwa ‘nyumbani.’
6
(b) Mahakama inaposhindwa kuamua
makazi rasmi ya mzazi au mlezi, mahakama itaamini kuwa makazi ya mzazi au mlezi
huyu ni yale yaliyopo katika eneo la Serikali ya Mtaa ambamo mtoto yumo au amepatikana.
Taasisi: maana yake ni makazi
yaliyoidhinishwa, makazi ya kizuizi, shule zilizoidhinishwa au taasisi kwa ajili
ya watoto wasio na makazi na watoto wa mitaani.
Inahusisha mtu au taasisi ya malezi
na udhibiti wa watoto.
Mahakama ya watoto: maana yake ni mahakama iliyoanzishwa
kisheria kuhusika na masuala ya watoto.
Waziri: maana yake waziri anayehusika na
masuala ya watoto.
Rafiki wa karibu: maana yake ni mtu anayeingilia kumsaidia
mtoto kuweza kufungua shauri mahakamani. Ina maana pia ya mlezi wa muda.
Yatima: maana yake ni mtoto ambaye amepoteza
wazazi wake wote au mzazi mmoja kwa kifo.
Msajili mkuu: maana yake ni msajili wa Vizazi na
Vifo. Msajili Mkuu anateuliwa kulingana na sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo.
Makazi ya kizuizi: maana yake ni mahali ambapo mtoto
hupewa makazi kwa muda wakati shauri dhidi yake likiwa linasikilizwa.
7
Ndugu: maana yake ni babu, bibi, kaka, dada,
binamu, shangazi au mtu yeyote ambaye ni mhusika katika ukoo wa kidugu.
Ofisa wa Ustawi wa Jamii: maana yake ni ofisa wa Ustawi wa
Jamii katika utumishi wa serikali.
No comments:
Post a Comment