Thursday, June 28, 2018

TUTEKELEZE MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGs) [SEHEMU YA PILI]


Mara baada ya kuona lengo namba 1 hadi namba 5 katika makala iliyopita. Sasa tutazame lengo namba 6 hadi namba 10. Je unafahamu lengo namba 6 linahusu nini? vipi kuhusu lengo namba 7,8,9, na 10?, Utekelezaji wake ukoje? Basi karibu uungane nami katika mfululizo huu wa darasa kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).


Maji Salama na Usafi
Watu husema Maji ni Uhai, na Usafi ni Maisha.  Maji salama na usafi ni lengo la sita ambalo linaweka msisitizo katika upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na usafi kwa wote. Limelenga kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa watu wote ifikapo mwaka 2030. Hivyo linasisitiza jamii zote duniani kuhakikisha zinaongeza kasi katika kuongeza upatikanaji wa maji safi ya kunywa na kutumia kwa gharama nafuu, kupunguza uchafuzi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kemikali zenye sumu hazitiririki na kuathiri vyanzo vya maji, bila kusahau kuboresha maji taka kwaajili ya matumizi ya baadae.

Nchini Tanzania suala la upatikanaji maji salama na usafi limekuwa likifanyiwa kazi kwa kiwango chake, licha ya kutoonesha matokeo chanya mpaka sasa. Huduma ya upatikanaji maji safi na salama imekuwa ikiboreshwa kwenye maeneo mengi ya nchi lakini bado kumekuwa na kero ya ukosefu wa maji safi na salama. Kampeni ya kumtua mwanamke au mtoto wa kike ndoo, ilianzishwa kwenye maeneo mengi hapa nchini ikilenga kuhakikisha maji yanapatikana kwa karibu zaidi ili kumpunguzia kero mtoto wa kike kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.

Kwenya baadhi ya mikoa kama Dar es Salaam wameweka mfumo wa kuwawezesha wananchi kuunganishiwa maji kwa mkopo ili kuhakikisha wananchi wake wanaendelea kupata huduma ya maji huku wakifanya malipo polepole, jambo ambalo limesaidia wananchi wengi wasiokuwa na uwezo nao kupata fursa ya kunufaika na huduma ya maji. Kwa hili, mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kuwa mkoa wa mfano katika kutekelza Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kuhusu suala la usafi, kumekuwa na kampeni za kuhamasisha usafi katika maeneo yote ya nchi, kampeni ambazo ziliasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika miezi ya awali kabisa ya uongozi wake.  Katika kuunga mkono kampeni hii, mkoa wa Dar es Salaam uliandaa kampeni maalumu ya kusafisha jiji hilo ambalo awali lilikuwa likiongoza kwa uchafu hapa nchini, kampeni hiyo imeonesha mafanikio kwa kiasi chake ambapo kwasasa maeneo mengi ya jiji hilo la kibiashara ni masafi tofauti na hapo awali.

Licha ya mafanikio hayo kiduchu katika utekelezaji wa lengo hili, kero za ukosefu wa maji zimeendelea kuripotiwa kutoka kila kona ya nchi. Huku hali ikisemekana kuwa mbaya zaidi katika mikoa ya Kigoma, Singida, na Shinyanga. Hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika kuhakikisha maji salama yanapatikana kwa wananchi wote wa Tanzania.


Nishati Mbadala kwa Gharama Nafuu
Lengo hili limelenga kuhakikisha nishati mbadala kwa gharama nafuu inapatikana ili kumwezesha kila mmoja kumudu gharama zake. Nishati hiyo pia inategemewa kuwa endelevu na ya kisasa kwa watu wote. Serikali na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kuhakikisha zinapunguza matumizi ya nishati inayotokana na misitu.

Matumizi ya umeme wa uhakika unaotokana na nishati mbadala kama jua, upepo, na gesi yanasisitizwa. Hii itasaidia pia kuepusha hatari ya kutokea kwa jangwa kutokan na ukataji miti hovyo kwaajili ya kupata kuni za kupikia na kuchoma mkaa.

Nchini Tanzania jitihada mbalimbali zimefanywa na zinaendelea kufanywa katika kuhakikisha lengo hili linafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Wizara ya Nishati imeendelea kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi kupitia miradi yake mbali mbali, ukiwemo mradi wa REA ambao umekuwa ukisambaza umeme vijijini kwa gharama nafuu zaidi.

Licha ya upatikanaji wa nishati ya gesi hapa nchini, nishati hii haijaweza kuwasaidia wananchi kwani matumizi yake ni ya kiwango cha chini, pia upatikanaji wake umeendelea kuwa ghari licha ya nishati hiyo kupatikana hapa nchini. Inasikitisha zaidi kuona hata maeneo ya Mtwara ambako gesi inazalishwa wameendelea kutumia kuni huku gesi hiyo ikitumiwa  na wakazi wa miji mingine hapa nchini.

Licha ya serikali pia kujitahidi kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia watanzania wengi zaidi, maeneo mengi ya nchi yameendelea kubaki gizani bila huduma hiyo, huku baadhi ya maeneo ambayo tayari yana huduma hiyo yakiendelea kupata umeme husiokuwa na uhakika kufuatia katika katika umeme ya mara kwa mara ambayo imekuwa ikiyakumba maeneo hayo.

Ni wakati sasa wa serikali kuhakikisha inaongeza nguvu katika wizara ya nishati kwa kuitengea bajeti ya kutosha itakayoiwezesha kusimamia zoezi la usambazaji umeme katika maeneo mengi zaidi ya nchi. Ikimbukwe kuwa upatikanaji nishati mbadala ni suala lenye matokeo mtambuka kwani licha ya kutumika majumbani, umeme hutumika pia viwandani katika kuzalisha bidhaa mbalimbali na hivyo kuongeza pato la taifa.


Kazi zenye Staha na Ukuzaji Uchumi
Lengo hili linahimiza ukuaji endelevu wa kiuchumi wenye kujumuisha watu wote, huku kukiwa na uzalishaji wa ajira na kazi za staha kwa wote. Linahamasisha pia sera za maendeleo zinazosaidia shughuli za uzalishaji, ujasiriamali, ubunifu na uvumbuzi, huku likihimiza urasimishaji na ukuzaji makampuni na taasisi ndogo ndogo na za kati, ikiwa pamoja na kuhakikisha zinapatiwa huduma za kifedha.

Limedhamiria ifikapo mwaka 2030 kuwepo na ajira kamili na za uhakika kwa wanawake na wanaume wote, bila kusahau vijana na watu wenye ulemavu ikiwa sanjari na ujira sawa kwa kazi zenye thamani sawa. Linasisitiza pia suala la kupunguza kiasi cha vijana wasio na ajira, elimu au mafunzo ifikapo mwaka 2020.

Linahimiza pia nchi zote duniani kuchukua hatua za haraka na za ufanisi kuondoa kazi za kulazimisha, kukomesha utumwa wa kisasa na biashara ya binadamu. Suala la kukomesha aina zote za utumikiswaji watoto na matumizi ya wanajeshi watoto ifikapo mwaka 2025, limezungumziwa pia.
Lengo hili pia linazitaka nchi zote duniani kuhakikisha zinalinda haki za wafanyakazi na kuweka mazingira salama ya kazi kwa wafanyakazi wote, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wahamiaji, hasa wahamiaji wanawake, na wale walio katika kazi ngumu na hatarishi.

Nchini Tanzania utekelezaji wa lengo hili bado unasua sua. Tatizo la ajira kwa vijana limeongezeka mara dufu, huku vyuo vikiendelea kuzalisha wasomi na watalaamu ambao baada ya kuhitimu masomo yao wanasota mtaani bila kupata ajira toka serikalini. Utumikiswaji wa watoto katika shughuli mbalimbali ikiwemo kazi za nyumbani (ndani) umeendelea kuwepo licha ya hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na serikali kukomesha utumikiswaji wa watoto.

Haki za wafanyakazi bado hazifuatwi. Wafanyakazi wawekuwa wakisimamishwa na kufukuzwa kazi bila kufuatwa kwa utaratibu. Wengine wamekuwa wakikosa stahiki zao wanazostahili mara baada ya kuwa wamefutwa au kusimamishwa kazi. Ni wakati sasa kwa serikali ya Tanzania kutazama suala la haki za wafanyakazi hapa nchini, ikiwa pamoja na kuwaandalia mazingira mazuri ya kufanyia kazi.


Viwanda, Ubunifu na Miundombinu
Lengo hili linalenga kuhimiza nchi zote duniani kujenga miundombinu imara, kukuza viwanda jumuishi na endelevu, na kuchochea ubunifu (uvumbuzi). Limedhamiria kukuza miundombinu yenye ubora na kuaminika inayozingatia jiografia ya maeneo husika hasa vijijini ili kusaidia ustawi wa maendeleo ya kiuchumi kwa wote.

Linalenga pia kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, ikiwa pamoja na mikopo yenye masharti nafuu kwa viwanda vidogo vidogo, na kwa wazalishaji wengine. Jambo hili sharti liende sambamba na kuhakikisha masoko yanapatikana kwa ajili ya bidhaa zinazozalisha na viwanda hivi vidogo vidogo.

Lengo hili pia linazitaka nchi zote mwanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la upatikanaji wa habari na teknolojia ya mawasiliano, pamoja na huduma nafuu ya mtandao (internet) kwa nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2020.

Suala la uanzishwaji wa viwanda nchini Tanzania limefanikiwa kwa kiasi chake chini ya uongozi wa awamu ya tano ambao umeweka mkazo katika uchumi wa viwanda. Viwanda mbalimbali vimeanzishwa katika maeneo tofauti ya nchi ikiwemo mkoani Simiyu ambako wameanzisha kiwanda cha chaki kinachohudumia mkoa huo pamoja na maeneo mengine ya jirani.

Licha ya mafanikio hayo katika uanzishwaji viwanda nchini, dhana ya viwanda kwa wananchi wa Tanzania bado haijaeleweka vizuri, huku wananchi wakitaka ufafanuzi zaidi kuhusu dhana ya ‘kiwanda kwa vyerehani vinne’ kama ilivyoelezwa na mamlaka yenye kusimamia sekta ya viwanda nchini.


Kupunguza Tofauti
Lengo hili linalenga kupunguza hali ya kutokuwepo kwa usawa ndani na miongoni mwa nchi mbalimbali hapa duniani. Linasisitiza juu ya uwezeshaji na ushirikishwaji jumuishi wa shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa watu wote bila kujali umri, jinsia, ulemavu, ukabila, asili ya mtu, dini, hali ya kiuchumi, au hali yoyote ile.

Linalenga pia kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa fursa na kupunguza tofauti ya kimatokeo, ikiwa ni pamoja na kuondoa sheria, sera na taratibu za kibaguzi, na kuhamasisha sera na hatua zenye kuhimiza usawa kwa wote. Linasisitiza juu ya kuimarisha sheria na taratibu juu ya usimamizi wa masoko ya kifedha zitakazokuwa na sura ya usawa kwa mataifa yote.

Linadhamiria pia kuhakikisha kunakuwepo na uwakilishwaji sawa katika kufikia maamuzi ya masuala mbalimbali ya kimataifa ikiwemo uchumi na fedha ili kujenga mazingira ya uwazi na uwajibikaji kwa mataifa yote. Vilevile linasisitiza juu ya kutekelezwa kwa sera zenye kutoa upendeleo maalumu wa huduma kwa nchi zinazoendelea kwa kuzingatia makubaliano na shirika la biashara duniani.

Nchini Tanzania bado kumeendelea kuwepo na tofauti kubwa ya kimaendeleo kati ya maeneo ya mjini na vijijini, hali inayoonesha kutofanikiwa kwa lengo hili hapa nchini. Huduma za kijamii na kiuchumi kama barabara zimebaki kuwa changamoto kubwa katika maeneo mengi ya vijijini ukilinganisha na maeneo ya mjini.

Wakati wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakifurahia usafiri safi na wa haraka wa mwendo kasi, hali ni tofauti kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma ambao hawategemei kabisa kupata huduma hiyo katika kipindi hiki. Huduma za kifedha kama benki bado hazijafika kwenye baadhi ya maeneo ya vijijini na hivyo kuwalazimu wakazi wa maeneo husika kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za kifedha.

Mara baada ya kuangalia lengo namba 6 hadi namba 10, Je kwa upande wako una nini cha kuongezea kuhusu malengo haya? Je, ni kweli hakuna mtu aliyeachwa nyuma katika utekelezaji wa malengo haya?, Je wewe binafsi upi ni mchango wako katika kuhakikisha kuwa hadi ifikapo mwaka 2030 malengo haya yanakuwa yametekelezwa kikamilifu?

No comments:

Post a Comment

FAHAMU KUHUSU MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGs)


SHULE INAYOTOA MICHEZO KAMA HII INAFAA KWA MZAZI NA MLEZI KUPELEKA MTOTO WAKE